• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 23, 2016

  YANGA 'MIGOMO' WALAZIMISHWA SARE 1-1 NA AFRICAN LYON

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA imevuna faida ya mgomo baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Matokeo hayo yanaifanya Yanga iendelee kukamata nafasi ya pili kwa pointi zake 37 baada ya kucheza mechi 17 sawa na Simba iliyo kileleni kwa pointi zake 38.  Simba inaweza kuongeza gepu la pointi hadi nne iwapo itashinda dhidi ya JKT Ruvu leo Uwanja wa Uhuru. 
  Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao na African Lyon walicheza kwa kujihami zaidi kipindi cha kwanza wakifanya mashambulizi ya kushitukiza.
  Mashambulizi ya Yanga leo hayakuwa na nguvu kutokana na kocha Mzambia, George Lwandamina kulundika viungo watano, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Said Juma na Deus Kaseke akitumia mshambuliaji mmoja tu, Amissi Tambwe.
  Kiungo wa Yanga, Mzimbabwe Thabani Kamusoko akikosa bao la wazi leo 
  Kiungo wa Yanga, Deus Kaseke (kulia) akitafuta maarifa ya kumpira beki wa Lyon, Miraj Adam 
  Winga wa Yanga, Simon Msuva akimiliki mpira mbele ya beki wa African Lyon

  Hata hivyo, ililitia misuokosuko lango la Lyon kuanzia dakika ya tatu baada ya Tambwe kupiga kichwa vizuri akimalizia krosi ya Msuva, lakini mpira ukaenda juu kidogo na dakika ya 33 Niyonzima akapiga juu ya kuikosesha timu yake bao la wazi.
  Lyon nayo ilikaribia kupata bao dakika ya 30 kama si mpira wa kichwa wa Thomas Maurice kwenda nje baada ya krosi ya Abdallah Mguhi ‘Messi’.
  Kipindi cha pili, timu zote ziliingia kwa malengo ya kutafuta mabao na kuanza kushambuliana moja kwa moja hali iliyonogesha mchezo. 
  Walikuwa Lyon waliofanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 67 kupitia kwa Ludovic Venance aliyemalizia pasi ya mchezaji wa zamani wa Yanga, Abdallah Mguhi ‘Messi’.
  Venance aliyesajiliwa dirisha dogo kutoka Mbao FC ya Mwanza, alifunga bao hilo baada kuingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Awadh Juma.
  Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana, kwani Yanga walifanikiwa kusawazisha dakika ya 74 kupitia kwa mkali wake mabao, Amissi Tambwe akimalizia krosi nzuri ya beki wa kulia Juma Abdul.
  Yanga wakaongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Lyon kusaka bao la ushindi, huku wachezaji walioingia kipindi cha pili, Emmanuel Martin na Geoffrey Mwashiuya wakiupasua vizuri ukuta mgumu wa wenyeji wao, lakini bahati mbaya hawakupata bao. 
  Wachezaji wa Yanga walicheza chini ya kiwango chao na dhahiri walionekana kuathiriwa na maandalizi hafifu kabla ya mechi hiyo – hususan kutokana na mgomo wa mazoezi kwa siku mbili, Jumatatu na Jumanne wakishinikzia kulipwa mishahahra yao ya Novemba.
  Mashabiki wa Yanga waliwatukana wachezaji kwa kitendo cha kugoma na hawakufanikiwa kuwafanyia fujo kutokana na ulinzi wa askari.
  Kikosi cha African Lyon kilikuwa; Youthe Jehu, Baraka Jaffary, Miraji Adam, Halfan Twenye, Hamad Wazir, Hamad Manzi, Hassan Isihaka,Omary Abdallah/Peter Mwalyanzi dk80, Awadhi Juma/ Ludovic Venance dk46, Thomas Maurice/Cossmas Lewis dk82. na Abdallah Mguhi.
  Yajnga SC; Deogratias Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Haruna Niyonzima, Mwinyi Hajji Mngwali/Geoffrey Mwashiuya dk74, Kelvin Yondan, Vincent Bossou, Simon Msuva, Thabani Kamusoko/Obren Chirwa dk56, Amissi Tambwe, Said Juma na Deus Kaseke/Emanuel Martin dk65.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA 'MIGOMO' WALAZIMISHWA SARE 1-1 NA AFRICAN LYON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top