• HABARI MPYA

  Jumapili, Desemba 25, 2016

  YANGA SASA WADAI MILIONI 420 ZA AZAM TFF

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KATIKA hali inayoashiria ni kuyumba kiuchumi, klabu ya Yanga imeandika barua Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikitaka ilipwe malimbikizo ya fedha zake za haki ya matangazo ya Televisheni ya Azam TV, Sh. Milioni 372.
  Kwa ujumla Yanga inataka ilipwe Sh. Milioni 422 pamoja na Sh. Milioni 50 za kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Yanga haikupewa zawadi yake ya kutwaa ubingwa wa Kombe la ASFC Mei mwaka huu ikiwafunga Azam FC 3-0 katika fainali Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga pia ilisusa kuchukua mgawo wa haki za matangazo ya Televisheni kwa miaka yote mitatu baada ya kutoridhia mkataba wa TFF na Azam TV.
  Lakini katika hali ya kustaajabisha ghafla Yanga wameibua na kuiandikia barua bodi ya Ligi ya TFF kuomba malimbikizo ya fedha zake hizo, Sh. Milioni 372. 
  Habari za ndani ambazo Bin Zubeiry Sports - Online imezipata zimesema kwamba Bodi ya Ligi baada ya kupata barua hiyo ya Yanga waliwajibu wakiitaka klabu hiyo kwanza iandike barua ya kuutambua na kuukubali mkataba huo wa Azam TV ndipo utaratibu wa malipo yao ufanyike.
  Bodi ya Ligi bado inasubiri sasa barua kutoka Yanga wakiikubali Azam TV kurusha matangazo ya mechi za Ligi Kuu ili utaratibu wa malipo yao uanze.
  Na hatua ya Yanga kudai fedha hizo inakuja katika kipindi ambacho kumekuwa na matatizo hadi ya kulipa mishahara ya wachezaji.
  Inadaiwa wachezaji wa Yanga walipitisha miezi mitatu bila kulipwa mishahara kati ya Julai na Septemba na hiyo inatajwa kama sababu ya timu kufanya vibaya kwenye mechi za Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika.
  Aidha, wiki iliyopita wachezaji wa Yanga waligoma kwa simu mbili kufanya mazoezi, Jumatatu na Jumanne wakishinikiza kulipwa mishahara yao ya Novemba.
  Kwa ujumla hali ya kiuchumi si njema ndani ya Yanga tangu kuondoka kwa waliokuwa wadhamini wakuu, kampuni ya Bia Tanzania (TBL) waliokuwa wakiidhamini klabu hiyo pamoja na mahasimu, Simba kupitia bia ya Kilimanjaro.  
  Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit alipotafutwa katika simu yake alisema hawezi kuzungumza chochote kwa leo kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.
  “Jamani hata siku za sikukuu pia mnatupigia simu?”alihoji Baraka na baada ya kuuliwa kuhusu klabu kuiandikia barua Bodi ya Ligi ya TFF kudai malimbikizo ya fedha za Azam TV, alisema; “We nani kakuambia, kwanza siwezi kuzungumza chochote nipo nje ya ofisi, nipigie kesho nikiwa ofisini,”alisema. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SASA WADAI MILIONI 420 ZA AZAM TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top