• HABARI MPYA

  Jumamosi, Desemba 31, 2016

  BEKI WA SIMBA AFIWA NA WATOTO WAKE WATATU SIKU MOJA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  LICHA ya kufiwa na watoto wake wote watatu, beki wa Simba SC, Juuko Murshid leo amesafiri na kikosi cha timu yake ya taifa, Uganda The Cranes kwenda Tunisia kuweka kambi ya kujiandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon.
  Kocha wa Uganda, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Juuko yuko kwenye msafara wa The Cranes pamoja na msiba mkubwa alioupata.
  Wiki hii ilianza vizuri kwa Juuko, baada ya mkewe, Ruth kujifungua pacha watatu, wawili wa kike ambao ni Hadija na Hajara na mmoja wa kiume, Murshid Jr.
  Pole kwa msiba mzito; Juuko Murshid (kulia) akiwa na mchezaji mwenzake wa Simba, Ibrahim Hajib

  Lakini usiku wa kuamkia leo mtoto wake wa kiume alifariki dunia na baadaye mapema leo, watoto wake wa kike wamefuatia siku tatu tu tangu wazaliwe na kuifanya nyumba ya Juuko iliyogubikwa na furaha kugeuka ghafla kuwa ya vilio na majonzi. 
  Juuko Murshid amepenya kwenye kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 wa Uganda kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Januari 2016 nchini Gabon. 
  Mapema jana, Micho alisema kwamba ameita wachezaji 26 kati ya hao, wachezaji 23 wameteuliwa moja kwa moja kuichezea Uganda kwenye AFCON ya kwanza baada ya miaka 39 na wanne ni wa akiba iwapo katika orodha ya awali itatokea mmoja ataumia au kupata dharula yoyote kabla ya kuanza mashindano.
  Kocha huyo wa zamani wa SC Villa ya Uganda, El Hilal ya Sudan, Orlando Pirates ya Afria Kusini, Yanga ya Tanzania na St George ya Ethiopia, amewataja wachezaji wanne wa akiba ni Watenga Isma, Mukiibi Ronald, Vitalis Tabu na Nsibambi Derrick.
  Na kikosi kamili kinachokwenda Tunisia kesho ni; Odongkara Robert, Ochan Benjamin, Jamal Salim Magola, Iguma Denislawyer, Wadada Nicholas, Ochaya Joseph, Batambuze Shafiq, Juuko Murushid, Isinde Isaac na Waswa Hassan. 
  Wengine ni Qanyi Timothy, Aucho Khalid, Azira Mike, Mawejje Tony, Kizito Geoffrey, Oloya Moses, Mutyaba Muzamil, Walusimbi Godfrey, Kizito Luwaga Wiliam, Lubega Edrisa, Shaaban Mohammed, Serunkuma Geoffrey, Miya Farouk, Sentamu Yunus, Massa Geoffrey na Onyango Denis.
  Uganda, ambayo mara ya mwisho ilishiriki AFCON  mwaka 1978 na kuingia Fainali ikafungwa na Ghana 2-0, imepangwa Kundi D pamoja na Ghana, Mali na Misri. 
  Kwa ujumla Uganda imecheza fainali tano za AFCON, zikiwemo za mwaka 1962 iliposhika nafasi ya nne, 1968, 1974 na 1976 ilipokomea hatua ya makundi mara zote.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BEKI WA SIMBA AFIWA NA WATOTO WAKE WATATU SIKU MOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top