• HABARI MPYA

    Tuesday, December 20, 2016

    WACHEZAJI YANGA WASITISHA MGOMO, WAAHIDIWA KULIPWA KABLA YA IJUMAA

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    HATIMAYE wachezaji wa Yanga wamesitisha mgomo wao uliodumu kwa siku mbili, baada ya kuahidiwa kulipwa mishahara yao ya Novemba kabla ya ijumaa.
    Mmoja wa wachezaji wa Yanga ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online usiku huu kwamba wamemaliza mgomo wao baada ya kuahidiwa kwamba wataingiziwa mishahara kabla ya mechi ijayo, Ijumaa dhidi ya African Lyon.
    “Tumemalizana, wametuambia kila kitu wataweka sawa na kabla ya mechi (Ijumaa) kila  mtu atakuwa amekwishaingiziwa mshahara wake,”amesema mchezaji huyo ambaye hakutaka kutajwa.
    wachezaji wa Yanga wamesitisha mgomo wao uliodumu kwa siku mbili, baada ya kuahidiwa kulipwa mishahara yao ya Novemba kabla ya Ijumaa

    Wachezaji wa Yanga kwa siku ya pili leo wameendelea na mgomo wa kufanya mazoezi wakishinikiza walipwe mishahara yao ya Novemba.
    Ni wachezaji wawili tu walioonekana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam asubuhi ya leo, kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na beki Oscar Joshua.
    Zaidi ya hapo walitokea makocha tu, George Lwandamina na Wasaidizi wake, Noel Mwandila Mzambia mwenzake na wazalendo, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli Jacob Onyango na Mtunza Vifaa Mohammed Omar ‘Mpogolo’.
    Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit alifika Uwanja wa Uhuru na kukutana na hali hiyo ya kushangaza na akaenda kuzungumza na Lwandamina baadaye Mwambusi na Hafidh.
    Baada ya hapo wote wakaondoka na leo asubuhi mazoezi hayakufanyika Yanga. 
    Mgomo huo ulianza jana ghafla Uwanja wa Uhuru, wachezaji wakiwa wamekwishavaa, wakagoma kuingia mazoezini.
    Mapema leo, uongozi wa Yanga ulikanusha kuwapo kwa madai ya mishahara ya Novemba na kudai kwamba wachezaji wanagoma wakitaka walipwe mapema mishahara ya mwezi huu, Desemba.
    “Kinacholeta matatizo hapa ni kubadilika kwa mfumo wa ulipaji, yaani badala mwishoni mwa mwezi, sasa tunalipa mwanzoni mwa mwezi. Sasa wachezaji wanataka mishahara ya Desemba walipwe mapema kwa sababu ya hizi sikukuu,”alisema Baraka akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI YANGA WASITISHA MGOMO, WAAHIDIWA KULIPWA KABLA YA IJUMAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top