• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 28, 2016

  YANGA YAIPUMULIA SIMBA, YAIGONGA NDANDA 4-0 UHURU

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Yanga SC wamejirudisha jirani kabisa na Simba SC baada ya ushindi wa mabao 4-0 jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzaia Bara.
  Yanga SC inafikisha pointi 40 baada ya ushindi wa leo na sasa inazidiwa pointi moja na watani wao, Simba SC ambao hata hivyo wana mchezo mmoja mkononi na watacheza na Ruvu Shooting kesho.
  Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Eric Onoca wa Arusha aliyesaidiwa na Michael Mkongwa wa Njombe na Janeth Balama wa Iringa, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 3-0.
  Bao la nne; Vincent Bossou (kushoto) akicheza na Simon Msuva kushangilia baada ya kufunga bao la nne  
  Mfungaji wa mabao mawili ya Yanga leo, Donald Ngoma (katikati) akimpongeza Amissi Tambwe baada ya kufunga bao la tatu
  Amissi Tambwe akishangilia bao lake
  Donald Ngoma akishangilia bao lake
  Domald Ngoma akilimi mpira mbele ya beki wa Ndanda, Bakari Mtama
  Winga wa Yanga, Emmanuel Martin akiwatoka wachezaji wa Ndanda
  Vincent Bossou akiruka juu kuifungia Yanga bao la nne

  Mshambuliaji Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma alifunga mabao mawili mfululizo kabla ya Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe kufunga la tatu na beki Mtogo, Vincent Bossou akafunga la nne kipindi cha pili.   
  Ngoma alifunga bao la kwanza dakika ya nne akimalizia kona ya Haruna Niyonzima na akafunga la pili dakika ya 21 akimalizia krosi ya Juma Abdul Jaffar.
  Mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Tambwe akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 25 kabla ya kuonyeshwa kadi ya njano kwa kwenda kukipiga teke kibendera cha kona wakati akishangilia bao lake.
  Kipindi cha pili, Yanga ilirudi kwa kujiamini zaidi na kuanza kucheza kwa utulivu ikimiliki mpira zaidi na kuwapoteza kabisa wapinzani.
  Pamoja na hayo, Yanga ililazimika kusubiri hadi zikiwa zimesalia dakika mbili ili kupata bao lake la mwisho siku ya leo, lililofungwa na Bossou kwa kichwa akimalizia kona ya beki wa kulia, Juma Abdul Jaffar.
  ⁠⁠Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Vincent Bossou, Kevin Yondan, Said Juma ‘Makapu’/Justine Zulu dk60, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Thabani Kamusoko dk70, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Emmanuel Martin/Geoffrey Mwashiuya dk77.
  Ndanda FC; Jeremiha Kisubi, Kiggi Makassy, Bakari Mtama, Paul Ngalema, Hemed Khoja, Salvatory Ntebe/Ayoub Shaaban dk40, Abuu Ubwa/Salum Minely dk53, Nassor Kapaman Salum Telela, Omar Mponda na Riffat Khamis.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA YAIPUMULIA SIMBA, YAIGONGA NDANDA 4-0 UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top