• HABARI MPYA

  Jumamosi, Desemba 31, 2016

  SIMBA: MAVUGO, BLAGNON HAWAKUCHEZA MECHI SABABU NI WAGONJWA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imetahadharisha haina tatizo lolote na wachezaji wake, Laudit Mavugo na Frederick Blagnon na kwamba kukosekana kwao kwenye mechi mbili zilizopita ni kwa sababu wagonjwa.
  Washambuliaji Mavugo kutoka Burundi na Blagnon kutoka Ivory Coast walikosekana wote katika michezo miwili iliyopita ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Simba ikishinda 1-0 kila mechi dhidi ya timu za jeshi, JKT na Ruvu Shooting.
  Na katika mechi hizo, kocha Mcameroon Joseph Marius Omog alimuanzisha mshambuliaji mpya, Pastory Athanas aliyesajiliwa dirisha dogo mwezi huu kutoka Stand United, ambaye pamoja na kucheza vizuri, lakini ilizua minong’ono juu ya kukosekana kwa Mavugo na Blagnon.
  Frederick Blagnon (kulia) hajaonekana kwenye mechi mbili zilizopita kwa sababu ni mgonjwa

   Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara aliiambia Bin Zubeiry Sports - Online jana kwamba wachezaji wote hao, Mavugo na Blagnon walikosekana kwenye mechi hizo mbili zilizopita kwa sababu ni wagonjwa. 
  “Hakuna tatizo lolote, hao wachezaji wote ni wagonjwa ndiyo maana hawakuwapo kwenye hizo mechi,”alisema Manara.
  Akifafanua, Manara alisema kwamba Blagnon anasumbuliwa na maumivu ya nyonga wakati Mavugo alikuwa anaumwa tumbo.
  Hata hivyo, Manara alisema wote hao wanaendelea vizuri na leo watakuwamo kwenye mafara wa timu unaokwenda Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi.
  Simba inahamia kwenye Kombe la Mapinduzi baada ya kujiweka pazuri kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting juzi, bao pekee la kiungo Mohammed ‘Mo’ Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 44 baada ya kucheza mechi ya 18 na kuendelea kuogoza Ligi Kuu kwa pointi nne zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC.
  Kikosi cha Simba kinachotarajiwa kuondoka leo ni makipa: Peter Manyika, Dennis Richard na Daniel Agyei.
  Mabeki ni Hamad Juma, Janvier Bokungu, Novaty Lufunga, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda na Method Mwanjali.
  Viungo ni Said Ndemla, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mwinyi Kazimoto, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Muzamil Yassin, James Kotei na washambuliaji Pastory Athanas, Juma Luizio, Mavugo na Blagnon.
  Simba imepangwa Kundi A pamoja na Taifa ya Jang’ombe, Jang’ombe Boys, KVZ na mabingwa watetezi, URA ya Uganda na itafungua dimba na Taifa ya Jang'ombe kesho Saa 2:30 usiku.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA: MAVUGO, BLAGNON HAWAKUCHEZA MECHI SABABU NI WAGONJWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top