• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 22, 2016

  LWANDAMINA AWATUNZIA HESHIMA WAPINZANI WA YANGA RAUNDI YA AWALI LIGI YA MABINGWA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa Yanga, Mzambia George Lwandamina amepingana na maoni kwamba Yanga imepangwa na vibonde katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
  Mabingwa wa Tanzania, Yanga SC wataanza na Ngaya de Mbe ya Comoro na Lwandamina amesema hiyo si timu ya kubeza kwa kuwa ratiba nzima ya Raundi ya Awali imehusisha timu zenye viwango sawa.
  “Droo iko sawa, wapinzani wetu si timu ya kubeza natarajia ushindani na tutahitaji maandalizi mazuri kabla ya mchezo huo,”amesema Lwandamina leo akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online.
  Kocha George Lwandamina (wa pili kushoto) amesema Yanga imepangwa timu ngumu Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 

  Yanga wataanzia ugenini wikiendi ya Februari 10 hadi 12 kabla ya marudiano wikendi ya Februari 17 hadi 19, mwaka huu na wakivuka hatua hiyo watakutana na mshindi kati ya Zanaco ya Zambia na APR ya Rwanda katika Raundi ya kwanza wakianzia nyumbani Machi 10 hadi 12 kabla ya marudiano Machi 17 hadi 19 mwakani, 2017.
  Lakini Lwandamina amesema hawezi kuzungumzia hatua inayofuata kukutana na mshindi kati ya Zanaco na APR kabla ya kuvuka mtihani uliopo mbele yake dhidi ya mabingwa w Comoro.
  “Siwezi kuzungumzia mechi hiyo, subiri wakati wake utakapofika ndipo nitaizungumzia kwa sasa tunaelekeza nguvu zetu kwenye mtihani uliopo mbele yetu,”amesema.
  Lwandamina aliyejiunga na Yanga mapema Novemba, anakabiliwa na changamoto ya kuipiku rekodi ya mtangilizi wake, Mholanzi Hans van der Pluijm ambaye mwaka huu aliifikisha Yanga hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutulewa na Al Ahly ya Misri.
  Yanga ikaangukia kwenye kapu la kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, ambako ilifanikiwa kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola na kuingia Kundi A pamoja na TP Mazembe ya DRC, MO Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana.
  Yanga ilishika mkia kwenye kundi hilo na uongozi ukaamua kuliongezea nguvu benchi la Ufundi kwa kumleta Lwandamina, ambaye msimu huu naye aliifikisha Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Zesco United kabla ya kutolewa na Mamelodi Sundwons iliyoibuka bingwa.   Pluijm sasa amekuwa Mkurugenzi wa Ufundi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: LWANDAMINA AWATUNZIA HESHIMA WAPINZANI WA YANGA RAUNDI YA AWALI LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top