• HABARI MPYA

    Thursday, December 29, 2016

    NGASSA SASA RUKSA KUCHEZA MBEYA CITY, ITC YAKE YAFIKA

    Na Mwandishi Wetu, MBEYA
    KIUNGO Mrisho Khalfan Ngassa sasa yuko huru kuchezea klabu yake mpya, Mbeya City ya hapa baada ya kupatiwa Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
    Mwenyekiti wa Mbeya City, Mussa Mapunda ameiambia Bin Zubeiry Sports - Online leo kwamba ITC ya Ngassa aliyekuwa anachezea Fanja ya Oman imefika nchini asubuhi ya leo.
    Mapunda amesema kwamba anawashukuru Fanja, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka Oman (OFA) ambao kwa pamoja wamefanikisha kupatikana kwa ITC hiyo.
    Mrisho Ngassa sasa yuko huru kuchezea Mbeya City baada ya kupatiwa ITC yake

    “Ni kweli tumeipata, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Shirikisho la Soka nchini, TFF, Chama cha Mpira cha Oman, hakika wamefanya kazi kubwa kufanikisha kupatikana kwa ITC  hii na pia naishukuru Fanja FC na watendaji wote kwenye timu yetu, tumekuwa na mawasiliano mazuri muda wote mpaka tumefanikiwa,” alisema. 
    Mapunda alisema kwamba kuchelewa kufika kwa ITC hiyo hakukuwa na msuguano wowote baina ya klabu hizo mbili, bali kilichokuwa kinatokea ni tofauti ya wakati na siku za ufanyaji kazi  kwenye ofisi kulingana na taratibu za nchi hizo mbili, yaani Oman na Tanzania.
    “Hakukuwa na msuguano wowote uliosababisha kuchelewa kwa ITC  hii, kilichokuwepo ni utofauti wa taratibu za kiofisi, mara nyingi Oman siku za Ijumaa na Jumamosi inakuwa ni mapumiko na huku kwetu Jumapili inakuwa mapumziko, hapo ndipo palikuwa panatuletea  mpishano, jambo jema ni kuwa tayari tumeipata na tunaweza kumtumia mchezaji kwenye michezo yote ya ligi na mingine ambayo inaihusu klabu yetu,” alisema.
    Katika hatua nyingine Mapunda alisema kwamba maandalizi kuelekea mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Sokoine mjini hapa yanaendelea vizuri na lengo lao ni kushinda baada ya suluhu katika michezo yao miwili iliyopita. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGASSA SASA RUKSA KUCHEZA MBEYA CITY, ITC YAKE YAFIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top