• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 28, 2016

  YANGA NA NDANDA FC LEO PATAMU SHAMBA LA BIBI, SI MECHI YA KUKOSA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC inashuka Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam leo kumenyana na Ndanda FC ya Mtwara katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikitoka kulazimishwa sare ya 1-1 na African Lyon katika mchezo uliopita Ijumaa iliyopita hapo hapo, Uwanja wa Uhuru.
  Ndanda yenyewe itaingia kwenye mchezo huo ikitoka kufungwa mechi zote mbili za mwanzo za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, 2-0 kila mchezo na Simba na Mtibwa Sugar.
  Kocha George Lwandamina akizungumza na wachezaji wake katika mazoezi ya jana Uwanja wa Uhuru
  Wakati Yanga imepania kuzinduka leo baada ya sare ambayo haikutarajiwa na Lyon – Ndanda nao wanataka kushinda leo japo watakuwa ugenini.
  Mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu baina ya timu hizo ulimalizika kwa sare ya 0-0 Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
  Lakini wakati huo kocha Mkuu wa Yanga alikuwa Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye sasa amekuwa Mkurugenzi wa Ufundi na sasa timu inaongozwa na Mzambia, George Lwandamina.
  Hata wakishinda mechi yao leo, mabingwa hao watetezi, Yanga hawataweza kuiondoa Smba kileleni zaidi ya kupunguza gepu la pointi hadi kubaki pointi moja kutoka nne. 
  Simba ipo kileleni na itaendelea kuwepo baada ya leo kwa pointi zake 41 za mechi 17, dhidi ya 37 za mabingwa wa misimu miwili iliyopita, Yanga. 
  Simba yenyewe itashuka dimbani kesho kumenyana na Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam pia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA NA NDANDA FC LEO PATAMU SHAMBA LA BIBI, SI MECHI YA KUKOSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top