• HABARI MPYA

  Jumanne, Desemba 27, 2016

  FARID APAA KESHO KWENDA HISPANIA KUANZA MAISHA MAPYA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WINGA wa kushoto wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid Mussa, anatarajia kuondoka nchini kesho Jumatano saa 5.00 usiku kuelekea nchini Hispania kujiunga na timu ya Deportivo Tenerife ya huko.
  Farid anaondoka kujiunga na timu hiyo ya Ligi Daraja la Kwanza Hispania kwa mkopo baada ya taratibu zote kukamilika ikiwemo kupata kibali cha kufanya kazi nchini humo.
  Akitoa taarifa rasmi ya klabu mbele ya waandishi wa habari, Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd, alisema kuwa anaondoka baada ya Tenerife kumtumia tiketi ya ndege tayari kabisa kwenda kujiunga nao.
  “Mchezaji Farid Mussa kama mnavyokumbuka tuliwaambia taratibu zake zinakwenda vizuri baada ya kukamilisha taratibu zote ubalozini, tunavyoongea na nyinyi hivi sasa ni kwamba klabu ya Tenerife imetuma tiketi ya Farid Mussa na anatarajia kuondoka kesho saa 5 usiku na ndege ya Shirika la KLM, atatoka Dar es Salaam, atapitia Amsterdam, Barcelona na baadaye Tenerife,” alisema.
  Idd alisema Azam FC inamtakia kila la kheri winga huyo katika safari yake mpya ya maisha soka huko aendako.
  “Kwanza tunamtakia kila la kheri, acheze kwa mafanikio na kuonyesha uwezo mkubwa ili iwe ni sehemu ya kufungua milango kwa wachezaji wengine kutoka Azam FC au klabu nyingine yoyote ya Tanzania,” alisema.
  Idd alichukua fursa hiyo pia kuzungumzia mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Tanzania Prisons utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex keshokutwa saa 1.00 usiku, ambapo amesema kuwa wanarejea nyumbani kuchukua pointi tatu muhimu baada ya kutoka sare mechi mbili zilizopita ugenini.
  “Ni mechi ngumu kisoka lakini katika mchezo wa awali tulikwenda Mbeya na tukawafunga Tanzania Prisons bao 1-0, ulikuwa ni mchezo mgumu na wa ushindani kwa hiyo tunarudi nyumbani kwa mara ya kwanza tangu tumeanza raundi ya pili hatujawahi kucheza nyumbani, hivyo ni matarajio yetu tunarudi nyumbani ili kufanya vizuri,” alisema.
  Azam FC inaelekea kwenye mchezo huo, ikiwa imejikusanyia jumla ya pointi 27 katika nafasi ya nne sawa na Mtibwa Sugar, ikizidiwa pointi 14 na vinara Simba waliojikusanyia 41, Yanga 37 na Kagera Sugar ikiwa nazo 28.
  Tayari Azam FC imeshathibitisha kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayofanyika visiwani Zanzibar kuanzia Desemba 30 hadi Januari 13 mwakani.
  Azam FC ambayo ni bingwa mara mbili wa michuano hiyo (2012, 2013), imepangwa Kundi B sambamba na Yanga, Zimamoto na Jamahuri, ambapo itaanza kufungua dimba Januari 2 kwa kuvaana na Zimamoto, mchezo utakaoanza saa 10.15 jioni ndani ya Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Akizungumzia ushiriki wa Azam FC, Idd alisema kuwa wanatilia mkazo michuano hiyo huku akidai kuwa benchi la ufundi la timu hiyo litatumia michuano hiyo kukiangalia kikosi chake na kuwaangalia vizuri nyota wapya wa kimataifa waliowasajiliwa kwenye dirisha dogo.
  “Tupo kundi moja na Yanga na hii ni mara ya pili mfululizo inatokea tunakutana nao kwenye kundi moja, tunaamini kuwa kundi letu litakuwa ndio lenye ushindani mkubwa, kila mtu anafahamu kuwa tunapokutana na Yanga aina ya mpira inakuaje na presha inakuaje kwa mashabiki, kwa hiyo ni matarajio yetu kutakuwa na ushindani mkubwa,” alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: FARID APAA KESHO KWENDA HISPANIA KUANZA MAISHA MAPYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top