• HABARI MPYA

  Jumanne, Desemba 27, 2016

  NAHODHA YANGA ASEMA SIMBA WANAONGOZA TU LIGI, UBINGWA BADO SANA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannaavaro’ amesema kwamba ni mapema mno kuiondoa Yanga kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online juzi, Cannavaro alisema kwamba baada ya Yanga kulazimishwa sare ya 1-1 African Lyon watu wengi wanaelekea kukata tamaa kama timu hiyo inaweza kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu.
  Cannavaro alisema watu wanaoikatia tamaa Yanga wakati huu lazima watakuwa wageni wa Ligi, kwani kwa uzoefu anaamini ligi bado mchichi.
  “Simba wametupita pointi nne, ambazo ni sawa na wastani wa mechi mbili na bado hawajacheza na sisi. Wakicheza na sisi tukawafunga, inabaki pointi moja, na wakitoa hata sare mechi nyingine watapoteza pointi mbili na sisi tutawapita,”alisema.
  Cannavaro alisema kwamba wachezaji wa Yanga kwa ujumla waliumizwa na sare ambayo hawakuitarajia dhidi ya Lyon, lakini sasa wanaelekeza nguvu zao katika mechi zijazo.
  “Kwa sasa hivi tunaelekeza nguvu zetu kwenye mchezo wetu ujao na Ndanda, tunahitaji kushinda kwanza ili kurejesha imani za mashabiki wetu na baada ya hapo tuendelee kupambana huku tukitazam na spidi ya wapinzani wetu (Simba) katika mbio za ubingwa,”alisema Cannavaro.
  Aidha, Nahodha huyo amewataka mashabiki, wapenzi na wanachama wa Yanga kuwa wavumilivu na wenye subira katika kipindi hiki na kushikamana na wachezaji wao ili kuwatia moyo wafanye vizuri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NAHODHA YANGA ASEMA SIMBA WANAONGOZA TU LIGI, UBINGWA BADO SANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top