• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 28, 2016

  AZAM YAWAFUKUZA WAHISPANIA WOTE, KALI ONGALA APEWA TIMU

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imemfukuza kocha wake Mspaniola, Zeben Hernandez Rodriguez na wasaidizi wake wote kufuatia matokeo mabaya katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Sasa, mchezaji wake wa zamani, Kalimangonga ‘Kali’ Sam Daniel Ongala ndiye atasimamia timu kumalizia msimu.
  Hata hivyo, inaelezwa, klabu ya Kali, Maji Maji ya Songea haijakubali kumuachia kocha wake huyo ambaye ana mkataba wa mwaka zaidi.
  “Maji Maji haijakubali kumuachia Kali, lakini mazungumzo yanaendelea, tunaamini tutafanikiwa kumtoa kule aje huku,”amesema kiongozi mmoja wa Azam FC, akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online jioni hii.  

  Kocha Mspaniola, Zeben Hernandez (katikati) akiwa na wasaidizi wake, wote wamefukuzwa Azam 

  Pamoja na kuipa timu Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga kwa penalty 4-1 kufuatia sare ya 2-2 Agosti 17, mwaka huu, lakini Rodriguez akashindwa kufanya vizuri katika Ligi Kuu.
  Katika mechi 17 hadi sasa, Azam imeshinda saba tu chini ya Rodriguez ikifungwa nne na sare sita, hivyo kukusanya pointi 27 na inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
  Kali pamoja na kuchezea Azam FC, pia alikuwa Kocha Msaidizi chini ya Muingereza Stewart Hall na Mcameroon Joseph Marius Omog.
  Rodriguez anaondoka na wasaidizi wake wote ambao ni Yeray Romero, Kocha Mkuu wa Viungo Jonas Garcia, Msaidizi wake, Pablo Borges, Kocha wa Makipa Jose Garcia na Daktari, Sergio Perez.
  Wahispania hao walianza kazi msimu huu wakimpokea Muingereza, Stewart Hall aliyeondolewa baada ya kushindwa kuipa timu ubingwa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM YAWAFUKUZA WAHISPANIA WOTE, KALI ONGALA APEWA TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top