• HABARI MPYA

    Wednesday, April 13, 2016

    YANGA YAIZIMA MWADUI TAIFA, AZAM YAIANGUSHA MTIBWA MANUNGU

    Na Saada Mohammed, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika mashindano ya nyumbani baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui FC jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Shukrani kwake, kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima aliyefunga bao la ushindi mwishoni kipindi cha pili, baada ya kubanwa kiasi cha kutosha na Mwadui.
    Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 56 baada ya kucheza mechi 23, ikiendelea kukaa nafasi ya pili nyuma ya Simba SC yenye pointi 57 za mechi 24. 
    Hadi mapumziko, timu timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
    Wafungaji wa mabao ya Yanga, SImon Msuva (namba 27) na Haruna Niyonzima (katikati) wakipongezana  

    Yanga walitangulia kupata bao kupitia kwa Simon Msuva aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Issoufou Boubacar.
    Mwadui walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 13 kupitia kwa mshambuliaji Kelvin Sabati aliyeukuta mpira uliopanguliwa na kipa Deo Munishi ‘Dida’ baada ya shuti lake mwenyewe.
    Bao hilo lilitokana na makosa ya kiungo Mzimbabwe wa Yanga, Thabani Kamusoko aliyepiga mpira ukanaswa na kiungo wa Mwadui, Razack Khalfan nje kidogo ya boksi akampasia Sabati aliyefunga.
    Baada ya bao hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na kosakosa za pande zote mbili.
    Winga wa Yanga, Simon Msuva (kushoto) akimiliki mpira pembeni ya beki wa Mwadui,David Luhende

    Kipindi cha pili, Yanga walianza kwa mabadiliko wakiwapumzisha Pato Ngonyani na Issoufou Boubacar na kuwaingiza Vincent Bossou na Godfrey Mwashiuya. 
    Refa Selemani Kinugani alimtoa kwa kadi nyekundu, Iddi Mobby dakika ya 70 kwa kumchezea rafu kiungo wa Yanga, Kamusoko.
    Yanga ikafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 86 likifungwa na kiungo Haruna Niyonzima kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya kichwa ya mshambuliaji Donald Ngoma kufuatia krosi ya beki Oscar Joshua.
    Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Pato Ngonyani/Vincent Bossou dk46, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Malimi Busungu dk79 na Issoufour Boubacar/Godfrey Mwashiuya dk46.  
    Mwadui FC: Shaaban Kado, Malika Ndeule, David Luhende, Iddy Mobby, Joram Mgeveke/Abdallah Mfuko dk30, Anthony Mataogolo, Jabir Aziz, Razack Khalifan, Kevin Sabati, Juma Mnyate na Hassan Kabunda/Nizar Khalfan dk57.
    Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Azam FC imeshinda 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
    Shukrani kwake, Nahodha John Raphael Bocco aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 62 kwa penalti baada ya mshambuliaji Kipre Herman Tchetche kuchezewa rafu kwenye boksi.
    AzamFC sasa inafikisha pointi 55 baada ya kucheza mechi 24, ikiendelea kukaa nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Simba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAIZIMA MWADUI TAIFA, AZAM YAIANGUSHA MTIBWA MANUNGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top