• HABARI MPYA

    Monday, July 06, 2015

    KUMPOROMOSHA DIAMOND NI SAWA NA KUZUIA MAFURIKO KWA MIKONO

    KUNA siku nilibahatika kumtazama Diamond Platnumz katika kipindi kimoja cha televisheni, akanigusa sana pale aliposema anaogo sana kurudi alipotoka.
    Diamond akafafanua kuwa kila akitazama historia ya maisha yake na hatua alizopitia, anapata woga wa kuyarudia maisha hayo na kwamba daima atajituma na kuhakikisha anasonga mbele badala ya kurudi nyuma.
    Ni Takriban miaka mitatu imepita tangu Diamond aliposema hivyo na tunachokiona leo ndicho alichokidhamiria na kukihitaji – Diamond yuko juu kimuziki, yuko juu kimaisha.
    Huyo ndiye Naseeb Abdul, dogo mpiganaji aliyepitia ‘misoto’ ya kila aina kwenye maisha yake.
    Kuanzia “Nenda Kamwambie”, “Mbalaga” hadi “Nana”, Diamond hajawahi kushuka, kila ngoma yake mpya ni zaidi ya jana, bei zake za show zinapanda maradufu na sasa sehemu pekee inayostahili kwa maonyesho yake kwa hapa nchini ni kwenye viwanja vya mpira na maeneo mengine kama hayo – enzi za kupiga kwenye kumbi za kuingiza watu 700 zimepita.
    Diamond wa leo ni wa kimataifa, kazi zake zinatambulika kimataifa, anashirikiana na wanamuziki wa kimataifa, anatesa kwenye media za kimataifa.
    Diamond wa leo ni pesa, kila atakachofanya ni pesa, akijitosa kwenye filamu ni pesa, akiamua kuandika kitabu cha maisha yake ni pesa, akitumia jina lake kwenye biashara ya mavazi au bidhaa zozote ni pesa.
    Nini tunachopaswa kukifanya kwa Diamond? Hakuna kingine zaidi ya kumuunga mkono na kumpa heshima inayostahili.
    Kuna nchi kibao zilizoendelea ambazo kila kukicha zinajaribu kuwalinda na kuwakuza ‘masupastaa’ wao wa fani mbali mbali wakiamini hao ni mabalozi wao wazuri popote pale duniani.
    Diamond hakubahatisha kufika hapo alipo bali ni kutokana na jitihada zake, uwezo wake, kipaji chake pamoja na nidhamu hali ya juu.
    Diamond sio mtu wa kupuuza kazi, sio mtu wa kupuuza vyombo vya habari, Diamond anajua namna ya kuwasiliana na dunia – ukitazama mashabiki wake wanamfuata kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na Instagram, utabaki ukiamini kuwa huyo si msanii wa kuporomoka leo au kesho, bado yupo sana kwenye ‘game’.
    Diamond ni aina ya wasanii wanaojifunza mengi kutoka kwa wasanii walipata mafanikio makubwa na kisha wakaporomoka na kubakia kuwa ‘pangu pakavu’ – hawana mbele wala nyuma.
    Wakati Diamond anapenya kwenye tuzo kibao za kimataifa ni vizuri tukamuunga mkono badala ya kumchafua na kumfanyia fitna zisizo na maana, kwa sasa Diamond amefikia hatua ambayo kama utamchukia utapata vidonda vya tumbo bure.
    Ipo tabia moja ya kibinaadamu ambayo inabidi ikemewe sana, nayo ni ile hali ya mtu aliye juu kuchukiwa, kwamba ili mwingine apande ni lazima kumshusha aliye juu na ili kumpandisha mwingine basi ni lazima atengeneze bifu na aliye juu - huu ni ujinga.
    Kila mfalme na zama zake, najua zama za Diamond nazo zitapita, lakini isiwe kwa fitna za kitoto, kufanya hivyo ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mikono – jamaa kishatusua, yuko matawi mengine.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KUMPOROMOSHA DIAMOND NI SAWA NA KUZUIA MAFURIKO KWA MIKONO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top