MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla jana alikutana, kuzungumza na kumpatia zawadi ya Viatu na vitu mbalimbali mchezaji Nyota na Winga wa TRA United Ramadhan Salum “Chobwedo”, akimsifu kwa kiwango chake bora na kikubwa alichokionesha katika Michezo ya ligi kuu Tanzania bara.
Mhe. Makalla ambaye pia ni mlezi wa Timu hiyo yenye makazi yake Mkoani Arusha, ameeleza kuwa Chobwedo ameonesha kiwango kizuri kwenye Mechi za TRA dhidi ya Yanga, Mechi zote mbili za Simba dhidi ya TRA zilizochezwa Dar Es salaam na Arusha pamoja na Mechi ya TRA dhidi ya Pamba, akimtaka pia kuwa makini na mitandao ya kijamii na asikubali ikawa sehemu ya kumvunja moyo kutokana na ukosoaji kadhaa wa watumiaji wa mitandao ya kijamii unaoelekezwa kwa mchezaji huyo.
“Mimi nimecheza mpira katika kiwango kikubwa lakini pia nimefundisha kwahiyo nikikupa sifa nakupa sifa za ukweli na nikisema hii ni Mali basi ni mali kweli, wewe Chobwedo ni Mali. Nimefuatilia mechi zenu nikiwa huko nje ya Nchi (Uturuki) nikasema nikuletee zawadi tena ya ‘bei mbaya’ (Kiatu chapa ya NIKE) na bei yake ni Dola 400 za Marekani ambayo ni zaidi ya Shilingi Milioni moja za Kitanzania, nikutakie kila la kheri na mimi nakutia moyo nenda kapambane.” Amesema Mhe. Makalla.
Kwa upande wake Nyota huyo wa TRA aliyetajwa kuwa mchezaji bora katika mechi kadhaa za hivi karibuni, amemshukuru CPA Makalla kwa malezi yake kwa Timu hiyo tangu ilipohamia Mkoani Arusha, akimshukuru pia kwa zawadi aliyompatia, akimuombea kheri kwa Mwenyenzi Mungu na kumuahidi kuendelea kupambana katika kutimiza malengo ya Timu yake ya TRA United.
Ramadhani Chobwedo amekuwa gumzo msimu huu akiwa na kiwango cha juu kabisa akiwa na TRA United, akishinda tuzo ya mchezaji bora wa mchezo (Man of the Match) zaidi ya mara tatu, akifanya hivyo dhidi ya Tanzania Prison, Yanga na Singida Big Stars, suala ambalo limesababisha tetesi kadhaa kwamba baadhi ya Vigogo wa Soka nchini Tanzania wamekuwa wakimuwinda.


.png)
0 comments:
Post a Comment