• HABARI MPYA

    Tuesday, June 09, 2015

    KAMA MABINGWA WENYEWE ‘FEKI’, AJABU GANI KUBORONGA MICHUANO YA AFRIKA?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    VIGOGO Tanzania wanashinikiza idadi ya wachezaji wa kigeni iongezwe kutoka watano wa sasa hadi saba- wakiamini wachezaji wa nyumbani hawana ubora wa kutimiza ndoto za klabu.
    Azam, Simba na Yanga SC ambazo kwa sasa zinagombea ubingwa na nafasi za kucheza michuano ya Afrika haziamini zinaweza kufika mbali kwa kuwa na wachezaji watano tu wa kigeni.
    Sasa, wamefanikiwa kulishawishi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liongeze idadi kutoka watano hadi saba na mchakato unaendelea ukiwa umefikia pazuri.
    Kipre Tchetche wa Azam FC akimtoka beki wa El Merreikh katika mchezo wa kwanza Raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu. Azam FC ilitolewa kwa jumla ya mabao 3-2. 

    Kikao cha Kamati ya Utendaji wiki iliyopita kiliiagiza Kurugenzi ya Ufundi ipitie maoni ya klabu juu ya hoja ya nyongeza ya wachezaji wa kigeni, na  baada ya hapo iwasilishe maoni yake Kamati ya Mashindano.
    Inaelezewa klabu zimependekeza wachezaji 10, lakini mpango uliopo ni kwamba TFF itakubali kila klabu itumie wachezaji saba kuanzia msimu ujao.
    Yote hii kwa sababu Azam FC, Simba na Yanga hazifiki mbali kwenye michuano ya Afrika na kwa kuzidiwa na wapinzani, zinaamini wachezaji wa nyumbani hawana ubora wa kuhimili michuano ya Afrika.
    Wanadhani, wakiwa na wachezaji wengi wa kigeni watakuwa na timu imara za kuleta hata Kombe la Afrika Dar es Salaam.
    Katika hoja zao wanatolea mfano zaidi TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), imekuwa tishio barani kwa sababu ya wachezaji wa kigeni.
    Mwaka 1974 Simba SC ikiwa na wachezaji wazalendo watupu chini ya kocha mzalendo pia, Paul West Gwivaha (sasa marehemu) lifika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa) ikiitoa timu ngumu ya Ghana, Hearts Of Oak katika Robo Fainali, tena ikiifunga 2-0 Accrah na kutoa sare Dar es Salaam   
    Simba SC hiyo ilikwenda kutolewa kwa mbinde katika Nusu Fainali na Mehalall El Kubra ya Misri kwa penalti baada ya sare ya jumla ya 2-2. 
    Na mwaka 1993, Simba SC ikiwa chini ya kocha mzalendo, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na wachezaji wazalendo watupu, ikafika Fainali ya Kombe la CAF.
    Mwaka 1969 na 1970, mahasimu wao, Yanga SC walicheza Robo Fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika mfululizo mara zote wakitolewa kwa ‘shida’ na Asante Kotoko ya Ghana.
    Mrisho Ngassa (kulia) akiichezea Yanga SC dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia kabla ya kuhamia Free State Stars ya Afrika Kusini mwishoni mwa msimu

    Lakini leo wachezaji wazalendo wanadharauliwa hawawezi kuzifikisha timu mbali. Tatizo nini? Hatutaki kutazama kiini halisi cha matatizo ya soka letu, badala yake tunatafuta majibu mepesi. 
    Kocha mkongwe nchini Nigeria, Lawrence Akpokona mwishoni mwa wiki amesema kwamba nchi hiyo haijawahi kuwakilishwa na klabu bora katika michuano ya Afrika.
    Kocha huyo wa zamani wa Crown FC, Bendel Insurance na Dolphins, alikuwa Uwanja wa Warri City akishuhudia wenyeji, Wolves wakitolewa katika Kombe la Shirikisho licha ya ushindi wa 3-1 dhidi ya AC Leopard ya Kongo. Wolves ilifungwa 3-0 mchezo wa kwanza.
    Na baada ya mchezo, akatoa maini yake akisema; 
    “Warri Wolves imetolewa (kwa matokeo ya jumla) kwa sababu walipoteza nafasi za kufunga mabao zaidi,” alisema.
    Dolphins ilikuwa timu nyingine ya Nigeria iliyotolewa katika Raundi ya kwanza ya michuano hiyo na Club Africain ya Tunisia.
    Enyimba na Kano Pillars pia zilitolewa mapema katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Akpokona amesema sababu ya matokeo hayo mabaya si siri tena.
    “Tatizo linaanzia katika ligi ya nyumbani. Lazima tuwe wakweli wakati tunapotafuta timu za kutuwakilisha kwenye michuano ya Afrika.
    “Klabu zisithubutu kufanya namna yoyote ili zishiriki michuano ya Afrika. Kwa ujumla klabu ambazo zinatuwakilisha katika michuano ya Afrika ni zile ambazo ziko vizuri kiuchumi.
    “Wakati mwingine, ni vigumu kufanikiwa kwenye ligi ya Nigeria, ikiwa hauna fedha.  
    “Ikiwa tutashughulikia hilo na mpira ukachezwa kama inavyotakiwa, maana yake klabu zitashinda nyumbani na ugenini, kisha tutakuwa na mabingwa wa ukweli wa kutuwakilisha kwenye michuano ya Afrika,” amesema mkongwe huyo.
    Wanigeria kwao wamegundua tatizo lipo katika mfumo wa Ligi yao- na japokuwa Akpokona hajaweka wazi sana, lakini unaweza kumuelewa.
    Kocha Lawrence Akpokona wa Nigeria

    Timu tajiri zinawezaje kutawala soka ya Nigeria kama si kwa sababu ya fedha zake? Na kwa sababu haziwi timu bora kwenye michuano ya Afrika, maana yake zinapanga matokeo.
    Hakuna ubishi, Tanzania klabu tajiri ni Azam, Simba na Yanga ambazo ndizo zinatawala soka yetu kwa sasa.
    Je, utawala wao ni soka au wanatumie fedha zao kupata matokeo mazuri kiulaini uwanjani? Sijui. Kusikia malalamiko ya marefa na wachezaji kuhongwa na timu pinzani hilo si jambo geni katika soka ya Tanzania. Na kama unakuwa na bingwa feki, ajabu gani matokeo mabaya michuano ya Afrika? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMA MABINGWA WENYEWE ‘FEKI’, AJABU GANI KUBORONGA MICHUANO YA AFRIKA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top