• HABARI MPYA

    Thursday, August 14, 2014

    KMKM YATOLEWA KOMBE LA KAGAME, YAPIGWA 1-0 NA RAYON KWA MBINDE KWENYE ‘MABWAWA’

    Na Mahmoud Zubeiry, KIGALI
    KMKM y Zanzibar imeipa mkono wa kwaheri michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya kufungwa bao 1-0 na wenyeji, Rayon Sport kwenye Uwanja wa Nyamirambo mjini hapa.
    Kwa matokeo hayo, KMKM inakamilisha mechi nne za kundi A ikiondoka na pointi mbili ilizovuna kwenye sare ya 1-1 mara mbili na Atlabara ya Sudan Kusini na Adama ya Ethiopia, huku mechi nyingine ikifungwa 4-0 na Azam ya Tanzania Bara.
    Kiungo wa KMKM, Ameir Khamis akimtoka beki wa Rayon kwenye madimbwi ya maji Uwanja wa Nyamirambo
    Ameir aliwasotesha sana mabeki wa Rayon kwenye madimbwi
    Rayon inapanda kileleni mwa kundi hilo, kwa kufikisha pointi saba baada ya mechi tatu, awali ikitoka sare ya 0-0 na Azam na kushinda 2-1 dhidi ya Adama.
    Katika mchezo wa leo uliochezwa kwenye mvua kubwa, bao lililoirudisha Unguja KMKM lilifungwa na beki wa kushoto Rayon, Abouba Sibomana dakika ya baada ya shuti lake la mpira wa adhabu ndogo kutoka umbali wa mita 22 kutinga moja kwa moja nyavuni.
    Sibomana alitumia mwanya wa wachezaji wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo kutopanga ukuta wao vizuri na kumtungua kipa, Mudathir Khamis aliyeshinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi kwa kazi nzuri leo.
    Kocha wa KMKM, Ally Bushiri ‘Bush’ alifanikiwa kuidhibiti Rayon kwa mfumo wa 4-5-1 na kufanya mchezo uwe mgumu kwa wenyeji- ingawa mvua ilipunguza ladha yake.
    Mvua iliongezeka dakika ya 30 na Uwanja ukajaa maji, kiasi cha mpira kushindwa kutembea, lakini refa Muhabi Alex wa Uganda, hakujali hilo na ngoma iliendelea kupigwa.
    Wakati wa mapumziko watu waliingia na mafagio kuondoa maji kwenye Uwanja huo wa nyasi bandia pamoja na gari maalum dogo mfano wa trekta.
    Ameir alijitahidi sana kuiongoza KMKM, lakini bahati haikuwa yao

    KMKM waligoma kuendelea na mchezo katika hali hiyo, lakini wakashinikizwa na kukubali kwenda kumalizia dakika 45 ambazo ziliwamaliza pia kwa kufungwa bao la SIbomana.
    Pamoja na kufungwa, KMKM walipoteza nafasi za wazi za kufunga zisizopungua tatu, moja Maulid Ibrahim ‘Kapenta’ aligongesha mwamba kipindi cha kwanza.
    Katika mchezo uliotangulia wa kundi hilo, Atlabara ilitoka sare ya 1-1 na Adama, wakati mchezo wa Kundi C, wenyeji wengine, Polisi walishinda 3-1 dhidi ya Benadir ya Somalia.
    Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi za Kundi B kati ya na wenyeji wengine APR watakaomenyana na Gor Mahia ya Kenya na Atletico ya Burundi na Telecom ya Djibouti, wakati Kundi C El Merreikh ya Sudan itakipiga na mabingwa watetezi, Vital’O.
    Maji yanatolewa uwanjani kwa trekta


    Hatua ya makundi ya michuano hiyo itahitimishwa keshokutwa kwa mechi za Kundi A kati ya 
    Adama City na Azam, Rayon na Atlabara, wakati Kundi B Telecom itamenyana na Gor Mahia na KCC na APR.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KMKM YATOLEWA KOMBE LA KAGAME, YAPIGWA 1-0 NA RAYON KWA MBINDE KWENYE ‘MABWAWA’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top