• HABARI MPYA

  Jumapili, Januari 26, 2014

  TUNA KILA SABABU YA KUMPONGEZA IVO MAPUNDA, WAPI MENGI MATUNDA?

  KAMA utaendeshwa mchakato wa kumchagua kipa bora kwa sasa Tanzania, bila shaka Ivo Mapunda atashinda kwa kura nyingi. Udakaji wake ndiyo kielelezo cha ubora wake na hakuna shaka hivi sasa nchni, yeye ndiye bora kuliko walinda milango wenzake wote.
  Lakini kila napomtazama Ivo, Napata picha ya mtu jasiri aliyepitia wakati mgumu kutokana na fitina za soka ya Tanzania, ambazo ziliwashinda makipa wengine wazuri kama Mengi Matunda wakaacha soka bado wadogo.
  Miaka mitatau iliyopita nilifanya mahojiano na kiungo Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima, nikamuuliza swali, je angependa mtoto wake pia acheze soka?

  Wakati namuuliza, jibu nililotarajia ni kwamba Haruna angeniambia ndiyo, atapenda mwanawe aendeleze jina lake kupitia soka, lakini ilikuwa tofauti.
  Alisema asingependa mwanawe acheze soka, kwa sababu huu ni mchezo wenye machungu mengi sana, ambayo hapendi mtoto wake akutane nayo.
  Ni kitu ambacho kilikuwamo akilini mwangu, lakini sikukitilia maanani, ila sasa nasema ni kweli, soka ni mchezo wenye machungu mengi sana.
  Hilo hata Abedi Ayew Pele, mwanasoka bora wa zamani Afrika pamoja na kuwarithisha wanawe mchezo huo, lakini anajua, soka ina machungu mengi.  Ndiyo, wakati fulani.
  Ila soka pia ina tamu nyingi pia. Kushinda mataji, kulipwa fedha nyingi, kuwafanya mamilioni washerehekee wakitaja jina lako, kuwa maarufu na tajiri.
  Lakini hayo, si sana kwa huku kwetu Afrika, hususan Tanzania. Soka ina machungu mengi sana na inataka moyo kumruhusu mwanao kucheza soka, ikiwa wewe ulicheza na umekutana na hayo machungu.
  Ivo alikuwa kipa wa Yanga kati ya mwaka 2006 na 2009 wakati akiwa pia kipa namba moja wa timu ya taifa ya Tanzania, chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo.
  Lakini aliachwa Yanga kwa hila na visa, akidaiwa kuihujumu timu hiyo, bahati nzuri kwake, kocha wa zamani wa timu hiyo, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ aliutambua ubora wake, akamuunganishia mipango ya kucheza St George ya Ethiopia.
  Ivo alicheza huko, akamaliza Mkataba akaja kucheza African Lyon kidogo, baadaye akaenda Kenya kuchezea timu ya Daraja la Kwanza Kenya, Bandari, aliyoipandisha Ligi Kuu na hatimaye kukuza thamani yake nchini humo, hata akasajiliwa na Gor Mahia.
  Akiwa Gor, umaarufu wake ulivuma na hatimaye Novemba mwaka jana kocha Kim Poulsen akamuita Taifa Stars na akaenda naye kwenye michuano ya CECAFA Challenge, ambako alifanya vizuri na kusajiliwa na Simba SC.
  Baada ya kusajiliwa Simba SC, kwa kipindi kifupi tu alichoifanyia kazi timu hiyo, tayari amekuwa kipenzi cha wapenzi wa timu hiyo na hakuna shaka yeye ni bora kuliko hata kipa Mghana wa timu hiyo, Yaw Berko.
  Lakini pamoja na hayo, kama Ivo asingekuwa mvumilivu, sasa hivi tayari zamani ameachana na soka.   
  Na hapo siwezi kujiuliza sana kwa nini simuoni uwanjani mtoto wa Golden Boy wetu wa miaka ya 1980, Zamoyoni Mogella ama mtoto wa Khalid Abeid au mtoto wa Leodegar Tenga.
  Na hapo hapo, naona ipo kila sababu ya kuwapongeza watu kama Abubakar Salum ‘Sure Boy’, Mao Mkami ‘Ball Dancer’ ambao leo vijana wao wanaendeleza majina yao uwanjani. Walikuwa wana moyo sana kuwaruhusu watoto wao kucheza, ikiwa wao walipambana na machungu ya soka ya Tanzania.
  Soka ya Tanzania imejaa majungu, fitina, dhuluma, wizi na uzandiki na katika haya yote, muathirika wa kwanza ni mchezaji. 
  Kabla ya kumlaumu mchezaji wa leo wa Tanzania kwa nini hachezi Ulaya kama wenzake wa nchi nyingine za Afrika, natazama mazingira yaliyomuibua na yanayomlea, sioni dalili za kumfikisha huko.
  Mchezaji anaibuka katika mazingira ya tabu sana, kucheza soka katika mazingira hatarishi, kutopewa sapoti za muhimu kama vifaa vya mazoezi, lishe bora na kadhalika.
  Na anapokuwa katika mazingira hayo hayo, hata akipata nafasi ya kusema ajaribu kutimiza ndoto zake, anakutana na changamoto nyingine za kumuumiza zaidi.
  Mungu amrehemu, Athumani Mambosasa, huyu alikuwa kipa hodari wa Simba SC miaka ya 1970 na moja ya sifa zake kubwa ni kudaka hadi kuiwezesha klabu hiyo kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974.
  Leo hii hata ukikutana na mashabiki wa Simba wale wa enzi hizo, si hawa wa leo oye oye, watakupa sifa za Mambo na ujasiri wake. Watakuambia sijui alitishiwa bastola aachie mabao Misri, lakini akagoma.
  Pamoja na sifa hizo, Mambo ameaga dunia hana furaha na Simba. Kwa nini? Alifukuzwa akiambiwa amehujumu timu. Mambo anakwenda kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980, alikuwa hana timu.
  Alikuwa amekwishaacha soka yupo zake Arusha amepumzika. Baada ya kufukuzwa Simba mwaka 1975, akidaiwa kuhujumu timu dhidi ya Yanga kipigo cha mabao 2-0 Zanzibar fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, siku hizi tunaita Kombe la Kagame, Mambo aliungana na wachezaji waliojitoa Yanga kufuatia mgogoro wa mwaka 1976 kwenda kuasisi timu ya Nyota ya Morogoro.
  Lakini wachezaji wa Yanga walipokuja Dar es Salaam kuasisi Pan Africans mwaka 1978, yeye akaamua kuacha soka.
  Taifa Stars ilipokuwa kambini Arusha kujiandaa na Fainali za Nigeria mwaka 1980, ndipo kocha akamkuta huko na kumuita mazoezini, akaridhika naye akaenda naye kwenye faianli hizo na aliporejea huko, akastaafu moja kwa moja.
  Mwameja Mohamed, pamoja na makubwa aliyoifanyia Simba kuipa mataji kibao na kuifikisha fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, lakini hadi leo nina barua yake ya kujiondoa Simba mwaka 1999 baada ya kusononeshwa na shutuma za kudaiwa kuhujumu timu.
  Lakini bado soka ina machungu mengi zaidi ya haya kuambiwa umehujumu timu. Muda mrefu mchezaji anakuwa mbali na familia yake, analazimika kujihimu kila siku kwa ajili ya mazoezi, mwili unachoka wakati mwingine, lakini anajituma.
  Zamani, kama mechi kesho, mchezaji hata akifiwa na baba au mama yake mzazi, kama timu inamtegemea haambiwi hadi baada ya mechi, ili aitumikie timu kwanza. 
  Wale maelfu wanaokwenda uwanjani ni kwa sababu ya wachezaji- sasa nenda kwenye suala la maslahi yao, hayo ni machungu mengine ya soka ya Tanzania.
  Mchezaji wa Ligi Kuu anamaliza miezi minne hajalipwa mishahara, wakati wengi wao ni vijana wadogo na wengine ni wanafunzi, wanatoka kwenye familia duni wanategemea fedha hizo hizo ziwasomeshe, maisha yakoje hapa?  
  Na hapo utastaajabu nini mwanasoka wa kimataifa wa zamani Tanzania anaomba nauli ya daladala? Sekilojo Chambua alipata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa Uarabuni mwaka 1998 akakataa ili aendelee kucheza Yanga, ila alipostaafu muulize alifanyiwa nini? Unaweza kumtoa machozi. 
  Kweli soka ina machungu mengi. Juma Kaseja amekuwa kipa wa kwanza Simba SC tangu mwaka 2003, akimpokea Mwameja Mohamed na amekuwa na mchango mkubwa sana kwenye timu hiyo, lakini mwaka jana kaachwa ‘kiroho mbaya’.
  Niliumia sana Mengi aliponiambia yeye mpira basi baada ya kuvurugwa na viongozi wa Yanga, wakidai eti alihujumu timu. Alikuwa kipa mzuri, ana umbo zuri na kwa umri ni mdogo wake Ivo, lakini akaamua bora auze mbao tu Tandale kuliko soka ya bongo. Tuna kila sababu ya kumpongeza Ivo Mapunda. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TUNA KILA SABABU YA KUMPONGEZA IVO MAPUNDA, WAPI MENGI MATUNDA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top