• HABARI MPYA

  Friday, January 24, 2014

  OKWI AITOA JASHO YANGA…SASA WAHAHA ILE MBAYA

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  YANGA SC wanahaha kumnasua mshambuliaji wao Mganda, Emmanuel Arnold Okwi aliyezuiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kucheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, hadi hapo ufafanuzi wa kesi yake na klabu ya Etoile de Sahel ya Tunisia utakapotolewa.
  TFF imesimamisha usajili wa Okwi Yanga wakati ikisubiri ufafanuzi kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa la (FIFA) juu ya kesi yake na Etoile.
  Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Januari 22, mwaka huu kupitia masuala mbalimbali, imesimamisha usajili huo baada ya kubaini kuwa Okwi aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka FIFA.
  Kaazi kweli kweli; Okwi kushoto akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Mussa Katabro kulia

  Okwi ambaye aliingia mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.
  Kamati imesema FIFA kuna kesi tatu kuhusiana na suala la mchezaji huyo, moja ni ya Okwi kuishitaki klabu hiyo kutomlipa mishahara, ya pili ya Etoile du Sahel kumshitaki Mganda huyo kwa utoro na ya tatu ya Simba kuishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000.

  a

  Hivyo, TFF imeiandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza Ligi nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake. 
  Lakini Yanga wanaamini walifuata taratibu zote kumsajili Okwi na kesi yake na Etoile kwa vyovyote haiwezi kumzuia kucheza Jangwani. Kwa sababu hiyo, Yanga wanataka barua rasmi kutoka TFF ili waiwasilishe FIFA itoe ufafanuzi mapema na mchezaji huyo aruhusiwe kucheza.
  Yanga inatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ashanti United, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na sasa ipo katika mapambano kuhakikisha inamnasua mchezaji huyo.     
  Tayari Yanga SC wana leseni ya mchezaji huyo kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, inayoanza mwezi ujao.
  Leseni ya Okwi iliyoambatana na taarifa ya klabu ya Yanga. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OKWI AITOA JASHO YANGA…SASA WAHAHA ILE MBAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top