• HABARI MPYA

  Jumanne, Januari 28, 2014

  BIFU LA OWINO NA LOGA SASA GUMU, UONGOZI SIMBA SC WANAWA, BORA MCHEZAJI AENDE KOCHA ABAKI

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  KOCHA wa Simba SC, Zdravko Logarusic ameendelea na msimamo wake mkali dhidi ya beki Mganda, Joseph Owino wa kutomtaka kikosini mwake kwa madai ya utovu wa nidhamu na ‘kujisikia’.
  Loga amewaambia vionozi wa Simba SC ana timu nzuri ya ushindi bila ya Owino na amemchomea zaidi mchezaji huyo kwa kusema, tangu ameanza kuifundisha timu hiyo Desemba mwaka jana, amekuwa tatizo kwake.
  Sitaki mchezaji jeuri; Kocha Logarusic ameendelea na msimamo wa kutomtaka Joseph Owino kikosini mwake

  Mcroatia huyo anamtuhumu Owino mambo mawili, kutofuata maelekezo yake na kujiona yuko juu ya kocha na wachezaji wenzake na kwa sababu hiyo anaona hafai kuwamo kwenye kikosi chake.
  Uongozi unampenda Owino, lakini hautaki kuingilia uamuzi wa kocha huyo na zaidi umekuwa ukimuombea msamaha mchezaji huyo kwa mwalimu huyo.
  “Loga anasema Owino ni tatizo na hata akimsamehe, ndani ya siku mbili tu atarudia matatizo yale yale. Na kilichomkera zaidi kocha ni mchezaji kuja kusema meneno ya uongo kuhusu yeye (kocha) kwa uongozi, kwa hiyo hamtaki kabisa,”kimesema chanzo kutoka Simba SC.
  Kuhusu haki za Owino kwa kuwa ana mkataba na Simba, inaonekana uongozi upo tayari kuvunja Mkataba na mchezaji huyo kwa sababu unaamini kocha ni bora kuliko mchezaji.
  Nimechoka kutukanwa tukanwa; Joseph Owino ameendelea kususia mazoezi Simba SC kwa madai anatukanwa sana na kocha Logarusic

  “Ila kwa kuwa jambo lolote siku za mwanzo linakuwa na moto, tunaendelea kuwapa muda, labda hasira zitaisha na watasameheana, ila kwa sasa hatuwezi kuingilia uamuzi wa kocha, hilo ni jambo la hatari sana,”kilisema chanzo.
  Owino alikorofishana na kocha Loga wiki iliyopita, akidai kutukanwa na mwalimu huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya na kujitoa mazoezini siku mbili kabla ya Simba kucheza mechi ya kwanza ya mzungkuo wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora Jumapili. 
  Na tangu wakati huo, Owino ameendelea kususia mazoezi Simba SC huku akipeleka malalamiko yake kwa uongozi kwamba hapendwi na kocha huyo.
  Loga anaipangua hoja ya kutompenda Owino kwa kusema amekuwa akimpanga mchezaji huyo tangu ameanza kazi Msimbazi pamoja na mapungufu yake na kama angekuwa hampendi asingekuwa anampa nafasi.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BIFU LA OWINO NA LOGA SASA GUMU, UONGOZI SIMBA SC WANAWA, BORA MCHEZAJI AENDE KOCHA ABAKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top