• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 22, 2014

  UBABAISHAJI, DHARAU SUMU YA SOKA YETU NA TUTANGOJA MILELE

  JANUARI mosi hadi 13 mwaka huu ilifanyika michuano ya soka ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, ambayo ilishirikisha na timu za nchi jirani, Kenya (Tusker na AFC Leopards) na Uganda (KCC na URA).
  Timu saba za Tanzania zilishiriki michuano hiyo, ambazo ni Azam FC, Simba SC iliyoingia Fainali na kufungwa na KCC 1-0, na Ashanti United za Bara na kwa upande wa visiwani, zilikuwepo KMKM, Chuoni, Spice Stars na Cloves Stars.
  Katika michuano kama hii, inaaminika ni sehemu nzuri kwa makocha wa timu za taifa kujitokeza kuangalia uwezo wa wachezaji kucheza mechi za ushindani.

  Ilikuwa michuano ambayo ilihusisha vijana wadogo kuanzia umri wa miaka 17, kutoka timu za pande zote mbili Bara na visiwani na kiasi kwamba makocha wa timu za vijana na ya wakubwa pia, Taifa Stars wangekuwepo ingewasaidia katika utendaji wao.
  Lakini kwa mastaajabu ya wengi, hakuna kocha yeyote wa timu yoyote, iwe ya vijana au ya wakubwa, angalau Msaidizi aliyeonekana Zanzibar, hadi siku ya fainali, kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen alipoibuka Uwanja wa Amaan, Simba SC ikimenyana na KCC ya Uganda.
  Lilikuwa ni jambo la kusikitisha sana, namna ambavyo ubabaishaji na dharau vimetawala katika soka ya nchi hii, kiasi kwamba huwezi kuona dalili za hata miaka 100 ijayo kupiga hatua yoyote kwa mwendo huu.
  Taifa Stars inakosa mchezaji mmoja muhimu sana beki wa kushoto, lakini kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi kulikuwa kuna mabeki wa nafasi hiyo zaidi ya saba, je kama Kim angejitokeza mapema angekosa japo mmoja?
  Labda angekosa kweli, lakini kushindwa baada ya kujaribu na kushindwa bila kujaribu, kipi bora? Bado tunasoma mwendo wa rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na timu yake, naona ana mambo mengi, anaonekana kutafuta suluhisho la matatizo ya soka yetu.
  Lakini kama anatumia njia ndefu sana, wakati soka ni mchezo wa kitaalamu hauhitaji ramli, ni suala la wataalamu kupewa majukumu wafanye kazi. Tuntaka kwenda Fainali zijazo za Kombe la Dunia, tutengenezewe programu na wataalamu ifanyiwe kazi.
  Hii ya kwenda kukaa semina na nini, sawa. Inaweza kuwa njia nyingine, lakini tayari soka ipo kitabuni na ina mwongozo wake, ni wa kuufuata tu, haya mengine kama si siasa ni ufujaji wa fedha tu.
  Mifano hai ipo, kuna nchi zilitengeneza programu kama Angola na wakazifuata, japokuwa ilichukua muda, lakini walivuna matunda yake kwa kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2006 nchini Ujerumani, ingawa baada ya hapo wakalewa sifa na kupotea mapema mno kwenye ramani ya soka ya kimataifa.
  Ghana na Ivory Coast wamekuwa watiifu, wameendelea kuzingatia programu zao na mwaka huu watacheza Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo, tangu walipocheza kwa mara ya kwanza kabisa nchini Ujerumani mwaka 2006. 
  Tumpe muda Malinzi na timu yake, ila kwa haraka haraka ni kama anatumia njia ndefu sana, lakini hili la makocha wa timu za taifa kupuuza Kombe la Mapinduzi linaashiria hawako makini na hawajui wanachokifaya.
  Hakuna sababu ya msingi, kama Kim hakuwepo, Msaidizi wake Sylvester Marsh alikuwepo. Lakini kwa nini Kim asiwepo wakati muhimu kama huo? Kweli kwa mwenendo huu, tujiulize tena na tena, tutafika kweli au ndiyo tutabakia kuwa mashabiki wa timu za wenzetu kwenye mashindano makubwa milele? Jumatano njema.
   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: UBABAISHAJI, DHARAU SUMU YA SOKA YETU NA TUTANGOJA MILELE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top