• HABARI MPYA

  Sunday, January 26, 2014

  SIMBA SC YAANZA VYEMA LIGI KUU, MESSI AFUNGA NA KUKOSA PENALTI, REFA SHAMBA AKATAA MABAO MAWILI YA TAMBWE

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  SIMBA SC imeanza vyema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ushindi huo, unaifanya Simba SC itimize pointi 27 baada ya kucheza mechi 14, ikibaki nafasi ya nne nyuma ya Yanga yenye pointi 31, Azam na Mbeya City pointi 30 kila moja. 
  Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na mshambuliaji Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’ dakika ya 14.
  Messi kulia akishangilia na wenzake baada ya kuifungia bao pekee Simba SC leo

  Messi alifunga bao hilo, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Rhino na ndipo akaupitia mpira na kufumua shuti kali lililoipa ushindi huo Simba SC.
  Pamoja na kufungwa, Rhino walicheza vizuri na kuonyesha upinzani kwa Simba SC ambao katika mechi ya mzunguko wa kwanza walitoka nayo sare ya 2-2 Uwanja wa Ally Hassan Mwinyhi Tabora. 
  Simba SC ingeweza kuondoka na ushindi mnene zaidi kama si refa Andrew Shamba wa Pwani kukataa mabao mawili ya Amisi Tambwe moja kila kipindi na Messi kukosa penalti dakika ya 70.
  Kwa nini alikataa? Beki wa Rhino akijaribu bila mafanikio kuuzuia mpira kwa mkono, lakini refa Andrew Shamba alikataa bao hili akidai Tambwe alimsukuma mchezaji huyo. 

  Penalti hiyo ilitolewa baada ya Haroun Chanongo kumnawisha mpira beki wa Rhino, Ladislaus Mbogo kwenye eneo la hatari. Messi pia alikosa mabao ya wazi mawili kipindi cha pili. 
  Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Idrisa Rashid, Gilbert Kaze, Donald Mosoti, Awadh Juma, Haruna Chanongo, Amri Kiemba, Ali Badru/Said Ndemla dk, Amisi Tambwe/Betram Mombeki dk65/Henry Joseph dk85 na Ramadhani Singano ‘Messi’.
  Rhino Rangers; Charles Mpinuki, Julius Masunga, Amani Juma, Ladislaus Mbogo, Laban Kambole, Hamisi Msafiri, Salum Kamana, Hussein Abdallah, Darlingtn Enyinna, Suleiman Jingo/Salum Majid dk84 na Shijja Mongo.
  Fundi wa mpira; Ramadhan Singano 'Messi' akimiliki mpira mbele ya beki wa Rhino 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAANZA VYEMA LIGI KUU, MESSI AFUNGA NA KUKOSA PENALTI, REFA SHAMBA AKATAA MABAO MAWILI YA TAMBWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top