• HABARI MPYA

  Thursday, January 23, 2014

  NGASSA APATA ZALI UTURUKI, SIMURQ PIK YATAKA KUMNUNUA, LAKINI YANGA WAMFANYIA ‘KITU MBAYA’

  Na Prince Akbar, Dar es Salaam
  MSHAMBULIAJI wa Yanga SC ya Dar es Salaam, Mrisho Khalfan Ngassa anatakiwa na klabu ya Simurq PIK ya Azerbaijani baada ya kuonyesha soka nzuri timu hizo zilipokutana Jumatatu nchini Uturuki katika mchezo wa kirafiki na kutoka sare ya 2-2.
  Hata hivyo, dili hilo tayari limeingia ‘kiza’ kutokana na uongozi wa Yanga SC kuitajia dau kubwa klabu hiyo, ambalo ni kama wameshindwa na kama wamesitisha nia ya kumsajili mchezaji huyo.
  Masikini Anko; Mrisho Ngassa amepata timu, lakini Yanga wametaka dau kubwa

  Chanzo cha habari kimesema kwamba, kiongozi wa Simurq aliambatana na mchezaji Mkenya wa klabu yake, Patrick Osiako kuongea na Mkuu wa msafara wa Yanga Uturuki, Salum Rupia, ambaye alitaja dau kubwa ambalo klabu hiyo imeshindwa kulimudu.
  “Jamaa wameshindwa, wametajiwa dau kubwa sana, ila walikuwa wana nia kabisa ya kumnunua Ngassa,”kilisema chanzo.  
  Mtoto huyo wa kiungo wa zamani wa Pamba ya Mwanza na Simba SC ya Dar es Salaam, Khalfan Ngassa alicheza vizuri Jumatatu na kufunga bao moja katika sare hiyo, lingine likifungwa na mshambuliaji wa Burundi, Didier Kavumbangu.
  Simurq PIK yenye maskani yake, Zaqatala msimu uliopita ilishika nafasi ya nne katika Ligi Kuu ya Azerbaijani na imewahi kucheza michuano ya UEFA ya Europa League mwaka 2009 ikatolewa katika hatua ya kwanza ya mchujo
  Yanga SC inatarajiwa kuondoka Uturuki leo, ilipokwenda Januari 10 na itafika Dar es Salaam kesho Alfajiri. Ilikuwa imeweka kambi katika hoteli ya Sueno Beach mjini Antalya kama mwaka jana na pamoja na mazoezi, pia ilipata mechi nne za kujipima nguvu na kushinda mbili na kutoa sare mbili. 
  Ilitoa sare mara mbili mfululizo, chini ya kocha wake Mkuu mpya, Mholanzi Hans van der Pluijm, 2-2 na Simurq Pik na 0-0 na KS Flumartari ya Albania.
  Awali, kabla Pluijm hajaanza kuinoa Yanga, ikiongozwa na kocha Msaidizi, Charles Boniface Mkwasa, ilishinda mechi mbili na kutoa sare moja kwenye kambi yake ya Uturuki kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na Ligi ya Mabingwa.
  Mabingwa hao wa Bara, walianza ziara ya Uturuki kwa sare ya 0-0 na KS Flamurtari Vlore kabla ya kuzifunga 3-0 Ankara Sekerspor na Altay SK 2-0 chini ya kocha Mkwasa, ambaye kwa sasa amerejea Tanzania kusherehekea miaka 25 ya ndoa yake.
  Pluijm alitua Uturuki na kuiona kwa mara ya kwanza Yanga ikiifunga 2-0 Altay na baada ya hapo akaanza kazi, na mechi yake ya kwanza alitoa sare ya 0-0 na KS Flumartari ya Albania na leo 2-2 na Simurq PIK.
  Yanga inatarajiwa kuanza mzunguko wa Pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi kwa kumenyana na Ashanti United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA APATA ZALI UTURUKI, SIMURQ PIK YATAKA KUMNUNUA, LAKINI YANGA WAMFANYIA ‘KITU MBAYA’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top