• HABARI MPYA

  Friday, January 24, 2014

  LALA SALAMA LIGI KUU BARA YAASHIRIA BINGWA ATAKUWA BINGWA KWELI

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  HATUA ya lala salama ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaanza wikiendi hii, kwa timu zote 14 kushuka dimbani ndani ya siku mbili, Jumamosi na Jumapili kuwania pointi tatu muhimu kuelekea mwisho wa msimu wa 2013 -2014. 
  Jumamosi, mabingwa watetezi waliokuwa kambini Uturuki kwa wiki mbili, watamenyana na Ashanti United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam FC watakuwa wenyeji wa mabingwa wa 1999 na 2000, Mtibwa Sugar ya Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Saalam.
  Yanga SC watatetea ubingwa?

  Coastal Union waliokuwa kambini Oman kwa wiki mbili pia, wataikaribisha JKT Oljoro Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Kaitaba, wakati Jumapili, Simba SC watakuwa watamenyana na Rhino Rangers ya Tabora Uwanja wa Taifa na JKT Ruvu watakipiga na ndugu zao, Mgambo JKT Uwanja wa Azam Complex.
  Ligi ya msimu huo imeonyesha kuwa na ushindani tangu mzunguko wa kwanza na kwa hakika ni vigumu kuthubutu kutabiri japo timu zipi zitashika nafasi tatu za juu, achilia mbali bingwa, ingawa Yanga, Azam na Mbeya City zilimaliza juu Novemba.
  Yanga SC iliongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya mechi za kwanza za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, kufuatia ushindi wa 5-1 dhidi ya Ashanti United, zote za Dar es Salaam.
  JKT Ruvu ikapaaa kileleni baada ya mechi za pili na ikadumu hadi mzunguko wa tano ilipoipisha Simba SC. Angalau Simba SC ilidumu kwa muda mrefu huko hadi mzunguko wa 10, ilipozipisha Azam FC na Mbeya City.
  Simba SC ikajivuruga na kujikuta inapotea kabisa ndani ya tatu bora, ikizipisha Azam, Mbeya City na Yanga SC.
  Yanga ikarejea kileleni baada ya mechi za mwisho za mzunguko wa kwanza, kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya JKT Oljoro, huku Azam na Mbeya City zikitoshana nguvu kwa sare ya 3-3.
  Mtambo wa mabao wa Azam FC; Kipre Tchetche anatarajiwa kuendelea kutamba kwa kufunga mabao Ligi Kuu akiwa na Azam FC
  Pointi 28 zikaifanya Yanga iliyoanzia kileleni baada ya mechi za kwanza kumalizia kileleni pia, ikizizidi kwa pointi moja moja Azam na Mbeya City.  
  Ivo Mapunda kipya wa Simba SC, anayetarajiwa kuisaidia timu hiyo kwa uhodari wake langoni

  Katika mechi 13, Yanga SC ilishinda nane, sare nne, ikafungwa moja na Azam FC, ikifunga mabao 31, kufungwa 11 na ikamaliza na pointi 28. Hata hivyo, kocha aliyeifanya Yanga imalize kileleni mwa Ligi Kuu, Ernie Brandts ametupiwa virago pamoja na wasaidizi wake wote, Freddy Felix Minziro na Razack Ssiwa na sasa timu ipo chini ya Mholanzi, mwingine, Hans van der Pluijm anayesaidiwa na Charles Boniface Mkwasa na Juma Pondamali.  
  Azam katika mechi 13, ilishinda saba, sare sita, haikufungwa hata moja, ilifunga mabao 23, ikafungwa 10, hivyo kumaliza na pointi 27. Lakini kocha aliyeifanya Azam imalizie hapo mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Muingereza Stewart Hall ametupiwa virago na sasa kuna Mcameroon, Joseph Marius Omog.
  Mbeya City iliyopanda msimu huu, katika mechi 13, ilishinda saba, sare sita, haikufungwa, imefunga mabao 19, imefungwa 10 na imemaliza na pointi 27. Hii ni timu pekee kati ya nne zilizo mstari wa mbele kwenye mbio za ubingwa ambayo inaendelea na kocha wake mzalendo Juma Mwambusi.
  Simba SC katika mechi 13, ilishinda sita, sare sita na kufungwa moja na Azam FC, imefunga mabao 26, imefungwa mabao 13 na ilimaliza na pointi 24. Simba SC imefukuza benchi zima la Ufundi baada ya mzunguko wa kwanza, chini ya kocha Mkuu Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na wasaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na James Kisaka, ambaye siku chache baadaye alifariki dunia. 
  Kagera Sugar katika mechi 13, ilishinda tano, sare tano na kufungwa tatu, imefunga mabao 15, imefungwa 10 na imemaliza na pointi 20. 
  Mtibwa Sugar katika mechi 13, ilishinda tano, sare tano, imefungwa tatu, imefunga mabao 19, imefungwa 17 na kumaliza na pointi 20.
  Ruvu Shooting katika mechi 13, ilishinda nne, sare tano na kufungwa nne, imefunga mabao 15 na imefungwa 15, hivyo kumaliza na pointi 17. Lakini Ruvu imepata pigo baada ya kocha wake Mkuu, Charles Boniface Mkwasa kuhamia Yanga pamoja na kiungo tegemeo, Hassan Dilunga. Wachezaji wake wengine wawili, mfungaji tegemeo, Elias Maguri na kiungo Ali Khan wapo Oman wanataka kujiunga na Seeb ya huko. Tayari timu hiyo ipo chini ya kocha Mkenya, Tom Olaba.
  Coastal Union walikuwa Oman, je itawasaidia kufanya vizuri lala salama Ligi Kuu?

  Coastal Union katika mechi 13, ilishinda tatu, sare saba na kufungwa tatu, imefunga mabao 10, imefungwa saba na ilimaliza na pointi 16. Coastal ilimfukuza kocha wake Hemed Morocco na sasa ipo chini ya Mkenya, Yussuf Chipo.
  JKT Ruvu katika mechi 13, ilishinda tano, haina sare zaidi ya kufungwa mechi nane, imefunga mabao 10, imefungwa 16 na imemaliza na pointi 15.
  Rhino Rangers katika mechi 13, timu hiyo iliyopanda msimu huu imeshinda mbili, sare tano na kufungwa sita, imefunga mabao tisa, imefungwa 16 na imemaliza na pointi 11.
  JKT Oljoro katika mechi 13, imeshinda mbili, sare nne, imefungwa saba, imefunga mabao tisa, imefungwa 19 na imemaliza na pointi 10. Itaingia mzunguko wa pili ikiwa na kocha mpya, Hemed Morocco aliyefukuzwa Coastal Union.
  Ashanti United katika mechi 13, imeshinda mbili, sare nne na kufungwa saba, wakati imefunga mabao 12, imefungwa 24 na imemaliza a pointi 10 pia. Katika benchi la Ufundi, imeongezewa nguvu na kocha mkongwe Abdallah Kibadeni aliyetupiwa virago Simba SC, ambaye atasaidiana na Nico Kiondo aliyekuwa na timu mzunguko wa kwanza. 
  Prisons katika mechi 13, ilishinda moja tu, sare sita na kufungwa sita, wakati imefunga mabao sita na kufungwa 16, ikamaliza na pointi tisa.
  Mgambo JKT, katika mechi 13, ilishinda moja tu, sare tatu na kufungwa tisa. Kichekesho zaidi, ilifunga mabao matatu, nayo ikifungwa 23.
  Karibu kila timu imekuwa na maandalizi mazuri kabla ya mzunguko wa pili, hali inayoashiria hatua hiyo itakuwa kali nay a kusisimua na bingwa atakayepatikana safari hii, atakuwa bingwa kweli. a
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LALA SALAMA LIGI KUU BARA YAASHIRIA BINGWA ATAKUWA BINGWA KWELI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top