• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 22, 2014

  ELIAS MAGURI AFELI MAJARIBIO OMAN

  Na Mahmoud Zubeiry, Muscat
  HABARI mbaya. Wachezaji wawili wa Ruvu Shooting ya Pwani, kiungo Ali Khan na mshambuliaji Elias Maguri waliokuwa wakifanya majaribio katika klabu ya Seeb ya Oman, wamefeli.
  Baada ya wiki mbili za mazoezi na timu hiyo pamoja na mechi mbili za majaribio, Seeb imeona wachezaji hao hawatawafaa na sasa inawaandalia safari ya kurejea Dar es Salaam.
  Bahati mbaya; Elias Maguri na mwenzake Ali Khan wanarejea Tanzania baada ya kufeli majaribio Oman
  Maguri ambaye alikuwemo kwenye kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kilichoshiriki Kombe la CECAFA Challenge mwaka jana, alicheza mechi mbili, wakati Khan alicheza mechi moja
  Mshambuliaji huyo aliyemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara akiwa na mabao manane nyuma ya kinara Amisi Tambwe Simba SC mabao 10, alicheza kwa dakika 45 wakati Seeb inamenyana na Coastal Union ya Tanga iliyo ziarani hapa Oman na hakufunga bao timu hizo zikitoka sare ya 0-0.   
  Maguri ni kati ya washambuliaji chipukizi nchini pamoja na Juma Luizio wa Mtibwa Sugar, ambao wanatarajiwa kuwa tegemeo la taifa miaka ijayo na pamoja na kufeli Seeb, hatakiwi kukata tamaa, bali kurejea nyumbani kuongeza juhudi na kujipanga upya.
  Wachezaji hao wanarejea nyumbani wakati mzuri, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ukianza Jumamosi ili waweze kuisaidia timu yao, ambayo tayari imempoteza kiungo wake hodari, Hassan Dilunga aliyehamia Yanga.
  Mechi tano zinatarajiwa kuchezwa katika miji ya Bukoba, Dar es Salaam, Tanga wakati mechi ya Ruvu Shooting na wenyeji Prisons inahamishiwa Uwanja mwingine.
  Ashanti United itacheza na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Coastal Union itacheza na Oljoro JKT katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Azam na Mtibwa Sugar.
  Jumapili kutakuwa na mechi kati ya JKT Ruvu na Mgambo Shooting itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex wakati Simba na Rhino Rangers zitaumana kwenye Uwanja wa Taifa.
  Mechi ya Prisons na Ruvu Shooting iliyokuwa ichezwe Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine inahamishiwa Uwanja mwingine kwa vile huo bado nyasi zake ambazo zimepangwa hivi karibuni hazijawa tayari kuhimili mechi hiyo.
  Prisons imetakiwa kutafuta Uwanja mwingine utakaaokidhi viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya mechi hiyo, na nyingine dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa Januari 29 mwaka huu.
   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ELIAS MAGURI AFELI MAJARIBIO OMAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top