• HABARI MPYA

    Monday, January 20, 2014

    YANGA YATOA SARE TENA UTURUKI CHINI YA BABU MHOLANZI, MKWASA AMEREJEA DAR NA USHINDI WAKE

    Na Baraka Kizuguto, Antalya
    TIMU ya Yanga SC ya Dar es Salaam imetoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Simurq PIK ya Azerbajain katika mchezo wake wa mwisho wa kirafiki kwenye ziara yake ya Uturuki, uliopigwa kwenye Uwanja wa Side Manavgat leo.
    Mabao ya Yanga katika mchezo wa leo yamefungwa na mshambuliaji wa Burundi, Didier Kavumbangu na mzalendo Mrisho Ngassa ‘Anko’.
    Mechi ya pili mfululizo hakuna ushindi, kwa nini Babu? Hans van der Pluijm ameiongoza Yanga kutoa sare kwa mara pili mfululizo Uturuki

    Dakika ya 13 ya mchezo mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Burundi, Didier Kavumbagu aliipatia Young Africans bao la kwanza kufuatia pasi nzuri ya mshambulaji Emmanuel Okwi na Didier kuukwamisha mpira wavuni na kumuacha mlinda mlango wa Simurq PIK Pawel Kapsa akiduwaa.
    Simuriq PIK walifanya shambulizi kupitia kwa kwa kiungo wao Stephan Polyak lakini golikipa wa Young Africans Juma Kaseja alikoa hatari hiyo, huku Tagim Novruzov akishindwa kumalizia mpira uliotoka sentimeta chache langoni.
    Dakika ya 30 ya mchezo Young Africans ilijipatia bao lake la pili kupitia kwa kiungo Mrisho Ngasa ambaye aliwatoka walinzi wa Simurq kufuatia migongeo mizuri katika Niyonzima, Okwi , Kavumbagu na kumkuta Ngasa ambaye aliukwamsiha mpira katika nyavu ndogo. 
    Kikosi cha Yanga SC leo
    Mpira wa krosi uliopigwa na nahodha wa Simurq Ruslan Poladov uliwapita walinzi wa Young Africans wakishindwa kuucheza na kumkuta mlinzi wa kati Anderson Oliveira aliyepanda kusaidia mashambulizi aliyeipatia timu yake bao la kusawazisha.
    Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwaza, Young Africans 2 - 1 Simurq PIK.
    Kipindi cha pili kilianza kwa Young Africans kufanya mabadiliko ambapo Nadir Haroub "Cannavaro" aliingia kuchukua nafasi ya Kelvin Yondani huku kiungo Hamis Thabit akichukua nafasi ya kiungo mkabaji Frank Domayo "Chumvi".
    Dakika ya 56 ya mchezo Simuriq PIK walipata bao la pili na la kusawazisha kupitia kwa mshambulaji wao Murad Sattarli baada ya kazi nzuri iiyofanywa na kiungo wao Stephan Polyak na mpira huo kuwapita walinzi wa Young Africans na kumkuta mfungaji.
    Mara baada ya bao hilo, timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu lakini mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 2 - 2 Simurq PIK.
    Huo unakuwa mchezo wa pili mfululizo, kocha mpya Mholanzi, Hans van der Pluijm anaiongoza Yanga bila kushinda tangu aanze rasmi kazi, baada ya awali kutoka 0-0 na KS Flumartari ya Albania.
    Awali, kabla Pluijm hajaanza kuinoa Yanga, ikiongozwa na kocha Msaidizi, Charles Boniface Mkwasa, ilishinda mechi mbili na kutoa sare moja kwenye kambi yake ya Uturuki kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na Ligi ya Mabingwa.
    Yanga SC ilianza ziara ya Uturuki kwa sare ya 0-0 na KS Flamurtari Vlore kabla ya kuzifunga 3-0 Ankara Sekerspor na Altay SK 2-0 chini ya kocha Mkwasa, ambaye kwa sasa amerejea Tanzania kusherehekea miaka 25 ya ndoa yake.

    Hongera Master; Mkwasa akiwa na mkewe, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa katika sherehe ya miaka 25 ya ndoa yao

    Pluijm alitua Uturuki na kuiona kwa mara ya kwanza Yanga ikiifunga 2-0 Altay na baada ya hapo akaanza kazi, na mechi yake ya kwanza alitoa sare ya 0-0 na KS Flumartari ya Albania na leo 2-2 na Simurq PIK.
    Yanga sasa imehitimisha mechi zake za kujipima nguvu na itaendelea na mazoezi hadi itakaporejea nchini mwishoni mwa wiki hii tayari kwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Ashanti United, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

    Kikosi cha Yanga kilikuwa; Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani/Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Frank Domayo/Hamisi Thabit, Mrisho Ngassa/Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Emmanuel Okwi na David Luhende/Said Bahanuzi.
    Simurq PIK: Pawel Kapasa, Ruslan Poladov, Dilaver Zrnanovich, Tural Axundov, Anderson de Oliveira, Tagim Novruzov, Nichat Kurbanov/Bashir Jamilu, Patrick Osiako, Salif Ballo, Rashad Ayyubov na Stepahn Polyak.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YATOA SARE TENA UTURUKI CHINI YA BABU MHOLANZI, MKWASA AMEREJEA DAR NA USHINDI WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top