• HABARI MPYA

    Thursday, January 30, 2014

    CHAN YAFIKIA TAMATI JUMAMOSI, GHANA NA LIBYA KUGOMBEA MWALI WA TATU CAPE TOWN

    Na Princess Asia, Johannesburg
    FAINALI ya michuano ya ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), mashindano yanayohusisha timu zinazocheza ligi za nchini mwao pekee inatarajiwa kupigwa Jumamosi wiki hii ikizikutanisha Ghana na Libya mjini Cape Town, Afrika Kusini.
    Ghana, au Black Stars wametinga fainali jana baada ya kuifunga Nigeria kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120 Uwanja wa Free State, Bloemfontein. 

    Ghana walicheza kwa dakika zaidi ya 50 wakiwa 10, baada ya Kwabena Adusei kupewa kadi ya pili ya njano na kuwa nyekundu, kufuatia kumchezea rafu Abubakar Ibrahim.
    Ghana ilifika Fainali ya CHAN mwaka 2009 na kufungwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lakini sasa kocha Maxwell Konadu amepata nafasi nyingine ya kujaribu kubeba taji hilo mbele ya Libya Februari 1 mjini Cape Town. 
    Libya ilikuwa ya kwanza kutinga Fainali baada ya kuifunga Zimbabwe kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 pia. Shujaa wa Libya alikuwa kipa Mohamed Abdaula aliyeokoa penalti ya mwisho ya  Zimbabwe kabla ya yeye mwenyewe kwenda kufunga penalti ya mwisho ya timu yake.
    Nigeria sasa itacheza na Zimbabwe kuwania Medali za Shaba mchezo utakaotangulia Jumamosi Saa 11:00 jioni kabla ya Ghana na Libya kuwania Kombe baadaye.
    Hii ni michuano ya tatu ya CHAN kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009, DRC wakiwa mabingwa wa kwanza kwa kuifunga Ghana 2-0 nchini Ivory Coast na mwaka 2011 Tunisia waliifunga mabao 3-0 Angola nchini Sudan. 
    Wachezaji wanachuana katika ufungaji bora ni Bernard Melvin Parker wa Afrika Kusini mwenye mabao manne, Rabiu Ali, Christantus, Uzoenyi Ejike wa Nigeria mabao matatu sawa na Abdelsalam Faraj Omar wa Libya na Junior Yunus Sentamu wa Uganda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHAN YAFIKIA TAMATI JUMAMOSI, GHANA NA LIBYA KUGOMBEA MWALI WA TATU CAPE TOWN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top