• HABARI MPYA

  Jumanne, Januari 21, 2014

  BABU MHOLANZI ATAMBA YANGA; “NINA WIKI MOJA TU KAZINI, LAKINI TIMU SASA INATISHA”

  Na Baraka Kizuguto, Antalya
  KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga SC ya Dar es Salaam, Mholanzi Hans van der Pluijm amesifu wachezaji wake jana walicheza vizuri kwa kufuata maelekezo yake wakitoa sare ya 2-2 na Simurq PIK katika mchezo wa kirafiki nchini Uturuki.
  Kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana, aliiambia tovuti ya Yanga jana kwamba, ana muda wa wiki moja tangu aanze kazi, lakini tayari anaona mabadiliko kiuchezaji na anategemea kufanya vizuri katika mashidano yanayomkabili.
  Timu imeiva; Kocha Hans van der Pluijm amesema Yanga sasa iko vizuri baada ya wiki moja ya kuwapo kwake kazini
  "Timu ilicheza vizuri, nawapongeza vijana kwa kujituma, hakuna lisilowezekana katika mpira, wachezaji wangu sasa hivi wanajiamini na wanajua wanatakiwa wafanye nini kwa wakati mwafaka, ilikua mechi nzuri sana, hata kocha wa Simurq PIK amefurahia uwezo wetu," alisema Pluijm.
  Huo ulikuwa mchezo wa pili mfululizo, kocha huyo mpya aliyerithi mikoba ya Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts akiiongoza Yanga bila kushinda tangu aanze rasmi kazi, baada ya awali kutoka 0-0 na KS Flumartari ya Albania.
  Basi wanalotumia Yanga Uturuki

  Awali, kabla Pluijm hajaanza kuinoa Yanga, ikiongozwa na kocha Msaidizi, Charles Boniface Mkwasa, ilishinda mechi mbili na kutoa sare moja kwenye kambi yake ya Uturuki kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na Ligi ya Mabingwa.
  Yanga SC ilianza ziara ya Uturuki kwa sare ya 0-0 na KS Flamurtari Vlore kabla ya kuzifunga 3-0 Ankara Sekerspor na Altay SK 2-0 chini ya kocha Mkwasa, ambaye kwa sasa amerejea Tanzania kusherehekea miaka 25 ya ndoa yake.
  Pluijm alitua Uturuki na kuiona kwa mara ya kwanza Yanga ikiifunga 2-0 Altay na baada ya hapo akaanza kazi, na mechi yake ya kwanza alitoa sare ya 0-0 na KS Flumartari ya Albania na leo 2-2 na Simurq PIK.
  Baada ya mechi ya jana ambayo ilikuwa ya nne kwa timu hiyo katika ziara yake ya Uturuki, Yanga itaendelea na mazoezi leo asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea nchini Alhamisi na itafika Dar es Salaam Ijumaa.
  Yanga inatarajiwa kuanza mzunguko wa Pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi kwa kumenyana na Ashanti United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BABU MHOLANZI ATAMBA YANGA; “NINA WIKI MOJA TU KAZINI, LAKINI TIMU SASA INATISHA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top