• HABARI MPYA

    Wednesday, January 29, 2014

    WAKATI MWINGINE MGUMU KWA SIMBA SC, LOGARUSIC…

    MACHO na masikio ya Watanzania wengi kwa sasa vimeelekezwa kwa kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic anayeifundisha Simba SC juu ya mustakabali wake kwenye klabu hiyo, kufuatia msimamo wake mkali kuwa kero kwa wachezaji wa klabu hiyo.
    Katika kipindi kifupi cha kufanya kwake kazi nchini tangu Desemba mwaka jana, Logarusic ameonyesha ni kocha mwenye misimamo mikali na asiyependa mzaha kazini. Hiyo inadhihirishwa na hatua anazochukua dhidi ya wachezaji wake, ambao wanaonekana kwenda kinyume cha mwongozo wake. 

    Jumapili, Simba SC ikimenyana na Rhino Rangers katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Logarusic alimtoa mshambuliaji Mrundi Amisi Tambwe dakika ya 65 na kumuingiza Betram Mombeki.
    Hata hivyo, dakika 20 baadaye akamuita nje Mombeki na kumuingiza Henry Joseph dakika ya 85. Hiyo ilionekana kumkera Mombeki na moja kwa moja akakumbuka Desemba 15, kocha huyo akiiongoza Simba SC katika mchezo wa kwanza kabisa, dhidi ya KMKM ya Zanzibar uliokuwa wa kirafiki.
    Siku hiyo, Logarusic alimtoa uwanjani dakika ya 30 mshambuliaji Mombeki, mara tu baada ya kukosa bao la wazi, kufuatia krosi nzuri ya Uhuru Suleiman kutoka upande wa kulia katika mchezo huo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo, ambao Simba SC ilishinda mabao 3-1, mguu wa Mombeki ulichelewa kugusa krosi ya Uhuru na ikapitiliza, huku akibaki ameshika kichwa kwa kutoamini kama amekosa bao la wazi.
    Wakati bado anatafakari namna alivyokosa bao hilo, akashituliwa kwamba anaitwa benchi kumpisha mshambuliaji mwingine, Tambwe Amisi.
    Lakini Logarusic kabla ya kumtoa Mombeki alimuita zaidi ya mara mbili kuzungumza naye kumuelekeza namna anavyotaka acheze, ila ni kama mshambuliaji huyo hakumfurahisha Mcroatia huyo aliyetua Simba SC kutoka Gor Mahia ya Kenya.  
    Mambo yalikuwa tofauti Jumapili, Mombeki baada ya kupewa pasi mbili na kupoteza Logarusic akamuamuru Henry avae jezi kwenda kuchukua nafasi.
    Loga alifanya hivyo siku mbili au tatu tu tangu akorofishane na beki Mganda, Joseph Owino mazoezini, ambaye ameamua kususia mazoezi. Owino amesusa kwa madai anatukanwa na mawalimu huyo, wakati Loga mwenyewe anasema  Mganda huyo ni jeuri na anajisikia yuko juu ya wengine wote hata makocha. 
    Uongozi wa Simba SC upo katika jitihada za kusuluhisha tofauti kati ya Owino na Loga, lakini kama itashindikana uko tayari kupoteza mchezaji na si kocha. 
    Desemba 21, mwaka jana wakati Simba inailaza Yanga 3-1 kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe, Logarusic alifanya mabadiliko ya mapema pia, akimtoa Said Ndemla dakika ya 27 na kumuingiza Ramadhani Singano ‘Messi’, aliyekwenda kucheza vizuri na kuwa chachu ya ushindi.  
    Pia siku hiyo, alimtoa Henry Joseph dakika ya 34, akamuingiza Ramadhani Chombo ‘Redondo’ ambaye alimtoa pia na kumuingiza Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ dakika ya 72,
    Tayari maneno yameanza, Loga akichukuliwa kama kocha mkorofi, lakini ukweli ni kwamba soka ya Tanzania inahitaji watu kama Mcroaita huyo ili kwanza kuweka sawa nidhamu za wachezaji.
    Lakini inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya wachezaji wanajipanga kupambana naye aonekane hafai. Sasa swali, watafanyeje ili kocha aonekane hafai kama si kucheza chini ya viwango vyao timu ifanye vibaya na uongozi uone Logarusic hafai?
    Hapa unaweza kuona Simba SC inaelekea kwenye wakati mwingine mgumu na wanahitaji kutumia hekima na busara kuhakikisha mgogoro wa kocha na wachezaji wote unamalizwa. Jumatano njema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAKATI MWINGINE MGUMU KWA SIMBA SC, LOGARUSIC… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top