• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 30, 2014

  OWINO AMUANGUKIA LOGA MBELE YA WACHEZAJI WENZAKE, ASAMEHEWA NA KUREJESHWA KUNDINI, LAKINI…

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  BEKI Joseph Owino amejishusha na kuomba radhi kwa kocha Zdravko Logarusic mbele ya wachezaji wenzake, juu ya tuhuma zake za utovu wa nidhamu na kujiona yuko juu ya wenzake- na bahati nzuri kwake amesamehewa na kurejeshwa kikosini.
  Habari kutoka ndani ya Simba SC zimesema kwamba, Owino aliandika barua ya kuomba radhi na baada ya hapo akaitwa kutakiwa kufanya hivyo mbele ya wachezaji wenzake pia, ili waridhie.
  Owino alipima kina cha maji kwa Logarusic, akagundua parefu hatimaye ameomba radhi na sasa amerejeshwa kundini

  Wachezaji wote wa Simba SC walipokea ombi la Owino kwa mikono miwili na kumkaribisha tena kundini, waendelee kupeperusha bendera nyekundu na nyeupe ya Mtaa wa Msimbazi.
  Lakini pamoja na kusamehewa, Owino atakatwa mshahara kwa siku zote ambazo hakuwa kwenye timu.
  Mcroatia huyo alikuwa anamtuhumu Owino mambo mawili, kutofuata maelekezo yake na kujiona yuko juu ya wachezaji wenzake na kwa sababu hiyo akaona hafai kuwamo kwenye kikosi chake, hadi akubali kubadilika.
  Owino alikorofishana na kocha Loga wiki iliyopita, akidai kutukanwa na mwalimu huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya, hivyo kujitoa mazoezini siku mbili kabla ya Simba kucheza mechi ya kwanza ya mzungkuo wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora Jumapili. 
  Na tangu wakati huo, Owino aliendelea kususia mazoezi Simba SC huku akipeleka malalamiko yake kwa uongozi kwamba hapendwi na kocha huyo.
  Loga akaipangua hoja ya kutompenda Owino kwa kusema amekuwa akimpanga mchezaji huyo tangu ameanza kazi Msimbazi pamoja na mapungufu yake na kama angekuwa hampendi asingekuwa anampa nafasi.   
  Mganda huyo sasa anatarajiwa kuanza mazoezi leo, tayari kwa mchezo wa mwishoni mwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: OWINO AMUANGUKIA LOGA MBELE YA WACHEZAJI WENZAKE, ASAMEHEWA NA KUREJESHWA KUNDINI, LAKINI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top