• HABARI MPYA

    Thursday, March 01, 2012

    ALL THE BEST YANGA, INAWEZEKANA


    KIKOSI cha wachezaji 20 wa Yanga kinaondoka leo na ndege ya Shirika la Egypt Air kuelekea Cairo, Misri tayari kwa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa soka Afrika dhidi ya wenyeji wao, Zamalek kwenye Uwanja wa Jeshi.
    Katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, timu hizo zilitoka sare ya kufunga bao 1-1, hali ambayo inailazimu Yanga kushinda mchezo huo ili iweze kusonga mbele.
    Kabla ya mechi hiyo kukubaliwa kucheza kwenye Uwanja wa jeshi kulikuwa na hofu ya kutofanyika jijini Cairo kufuatia mashabiki 74 kufariki uwanjani kutokana na vurugu kwenye mji wa Port Said wakati wa mechi ya Al Ahly na Al Masry.
    Mechi ya Yanga na Zamalek inafanyika bila watazamaji kutokana na wenyeji wao hao kupewa adhabu na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kucheza mechi zake za Ligi ya Mabingwa bila ya mashabiki kufuatia mashabiki wake kufanya vurugu wakati wa mechi dhidi ya Club Africain ya Tunisia msimu uliopita.
    Kutokana na sababu hizo msafara wa Yanga utajumuisha mashabiki 10 tu watakaoongozana na timu kwa ajili ya kuihamasisha.
    Akizungumzia mchezo huo, Kocha Kostadin Papic alisema wanafahamu wanakwenda kucheza mechi ngumu, lakini hilo haliwavunji moyo wa kucheza kwa kujituma na kupata ushindi.
    Papic alisema siku zote haamini katika kushindwa na kwa sababu hiyo anatarajia vijana wake watacheza kufa na kupona ili kurejea nyumbani na ushindi.
    "Nimejipanga kwa ajili ya ushindi na siyo kushindwa, makosa yaliyojitokeza katika mechi ya kwanza tumeshayarekebisha na sasa ni kupambana kwa nguvu," alisema Papic.
    Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Yanga, Selestin Mwesigwa alisema msafara wa timu hiyo utakuwa na watu 40 kwa mujibu wa maelekezo ya CAF.
    Mwesigwa alisema timu inakwenda ikiwa imekamilika vya kutosha, na wameridhika na maandalizi aliyofanya mwalimu kuelekea mechi hiyo.
    "Kama viongozi, tumefanya jitihada zote kuhakikisha tunaiandaa timu vizuri kwa ajili ya mechi hii. Kazi iliyobaki ni kwa wachezaji kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya mwalimu," alisema Mwesigwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ALL THE BEST YANGA, INAWEZEKANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top