• HABARI MPYA

    Tuesday, October 17, 2017

    RUVU SHOOTING YASHAURI BODI YA LIGI KUZIMULIKA TIMU ZINAZOSHINDA KILA MECHI NYUMBANI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Ruvu Shooting ya Pwani imeishauri Bodi ya Ligi, kuzimulika timu ambazo hazipotezi mechi nyumbani katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwani baadhi yao zinatumia njia haramu.
    Hayo yamesemwa na Masau Bwire, Msemaji wa Ruvu Shooting inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT) katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports - Online leo mjini Dar es Salaam.
    Bwire amesema timu zinazotegemea kushinda nyumbani kwa lazima ndizo zinazohujumu ligi, kwa sababu hutumia mbinu chafu kufanikisha malengo yao ya ushindi. “Hao wanaoshinda nyumbani kila mechi wamulikwe, ndio wanaovuruga Ligi, wanatumia mbinu chafu,”amesema.
    Amesema wao Ruvu Shooting si miongoni mwa timu zinazoshinda kila mechi nyumbani kwa sababu zinaacha haki itendeke na mshindi apatikane kutokana na jasho lake uwanjani. 
    Baada ya kucheza mechi sita bila kushinda, wakitoa sare tano na kufungwa moja 7-0 dhidi ya Simba, Ruvu Shooting, inayofundishwa na Abdulmutik Hajji ‘Kiduhu’ wanasafiri kuwafuata Mbeya City wikiendi hii Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Na Bwire amesema kwamba hana shaka watashinda mechi yao ya kwanza Jumamosi iwapo haki itatendekea Uwanja wa Sokoine.
    “Sisi tupo katika kiwango kizuri, kama mapungufu ni madogo tu ya wachezaji ambayo mwalimu anayafanyia kazi. Baadhi ya mechi tulinyimwa haki na marefa mfano dhidi ya Lipuli pale Iringa, ndiyo maana hatukushinda,”amesema.
    Bwire amesema wakishinda Jumamosi watajiinua mno kwenye msimamo wa Ligi Kuu kutoka nafasi ya saba hadi ya 13 walipo sasa kwa pointi zao tano.
    “Hii ligi bado mbichi sana, hadi sasa timu zenye pointi zaidi ya tisa ni sita tu (Simba, Mtibwa Sugar, Yanga, Azam zote pointi 12, Singida United 11 na  Tanzania Prisons 10), lakini sisi wengine wote ni chini ya tisa, maana yake sisi wenye pointi tano tukishinda mechi moja tunaweza kupanda hadi ya saba,”amesema.
    Kuelekea mchezo ujao, Ruvu Shooting itamkosa mchezaji wake Issa Kanduru aliyeonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Singida United pamoja na engine
    wanne wapo kwenye shughuli za kijeshi wakiwemo beki Damas Makwaya na mshambuliaji Fully Maganga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RUVU SHOOTING YASHAURI BODI YA LIGI KUZIMULIKA TIMU ZINAZOSHINDA KILA MECHI NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top