• HABARI MPYA

  Friday, October 20, 2017

  KADO AUMIA TENA MAZOEZINI MTIBWA SUGAR, AREJESHWA DAR KWA MATIBABU ZAIDI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIPA namba moja wa Mtibwa Sugar, Shaaban Hassan Kado ataendelea kuwa nje kwa angalau wiki mbili kwa matibabu zaidi baada ya kujitonesha goti katika mazoezi ya timu hiyo wiki iliyopita.
  Katibu Msaidizi wa Mtibwa Sugar, Swabur Abubakar ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam kwamba, Kado alijitonesha wakati wa mazoezi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba SC iliyofanyika Jumapili iliyopita timu hizo zikitoka sare ya 1-1.
  Abubakar amesema na baada ya mchezo huo, Kado ambaye awali aliumia kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Simba Agosti 13, mwaka huu Uwanja wa Uhuru akabaki Dar es Salaam kwa matibabu zaidi wakati timu ikirejea Morogoro.
  Shaaban Kado ataendelea kuwa nje kwa angalau wiki mbili kwa matibabu zaidi baada ya kujitonesha goti wiki iliyopita

  “Kwa suala la Kado tunatarajia kama atakuwa na wiki mbili nyingine za kuwa nje maana yake tumtarajie kuanzia wiki ya kwanza ya Oktoba atakuwa tayari kuanza kucheza tena,”amesema Abubakar.  
  Mbali na Kado, Abubakar amesema majeruhi wengine wa muda mrefu, beki Hassan Isihaka na kiungo Haroun Chanongo nao wanaweza kuwa nje kwa wiki mbili zaidi. “Wote wapo Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu na uongozi upo nao karibu sana kufuatilia mwenendo wa hali zao,”amesema.
  Aidha, Abubakar amesema kikosi cha Mtibwa Sugar chini ya kocha Zuberi Katwila kipo tayari kwa aili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons kesho Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
  Amesema timu imefanya mazoezi ya mwisho leo asubuhi na baada ya hapo wachezaji wamekwenda kupumzika kambini kujiandaa kisaikolojia kuwavaa Maafande wa jeshi la Magereza kutoka Mbeya.
  Mtibwa Sugar kwa pamoja na Azam FC, Simba, na Yanga SC zinafungana kwa pointi 12 kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kila timu kucheza mechi sita na mechi za wikiendi hii zinatarajiwa kuwatenganisha.  
  Mbali na Mtibwa kuwa wenyeji wa Prisons, Azam FC watakuwa wageni wa Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Yanga SC watakuwa wageni wa Stand United Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga Jumamosi pia na Simba SC watakuwa wageni wa Njombe Mji FC Jumapili Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KADO AUMIA TENA MAZOEZINI MTIBWA SUGAR, AREJESHWA DAR KWA MATIBABU ZAIDI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top