• HABARI MPYA

    Thursday, September 14, 2017

    KAMATI YABAINI MAPUNGUFU KIBAO LESENI ZA KLABU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetoa muda kwamba hadi Septemba 22, klabu zote 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na za zile  24 Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ziwe zimekamilisha taratibu za kupata Leseni za Klabu.
    Kwa mujibu wa Kamati ya Leseni za Klabu, ni timu tano za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya 16 hazikuchukua hata fomu za maombi ya Leseni za klabu wakati Klabu 11 zimebainika kuwa na upungufu mkubwa katika kukamilisha vigezo.
    Kamati ya Leseni za Klabu imekutana zaidi ya mara tatu katika vikao na kujiridhisha kwamba kwa ujumla vigezo vifuatavyo havijakamilika kwa asilimia 100 katika klabu nyingi kama zifuatavyo.
    Viongozi wa Azam FC, Mlezi Jamal Bakhresa (kulia) na Abdulkarim Amin 'Popat' (kushoto) klabu pekee iliyokamilisha taratibu za Leseni za klabu 
    1. Klabu zote hazina programu ya kuendeleza mpira kwa vijana.
    2. Taarifa za klabu haielezi kuhusu miundombinu ya kuhudumia walemavu wakati wa mchezo.
    3. Klabu hazijaonesha uwanja wa mazoezi.
    4. Hazijaambatanisha mikataba ya watendaji kama vile Katibu Mkuu; Ofisa Usalama wa timu, Mhasibu au mkurugenzi wa fedha, na daktari n.k.
    5. Taarifa hazina maelezo ya kocha wa timu za vijana.
    6. Klabu hazijajaza  fomu za kuomba Leseni ya klabu.
    7. Hazijambatanisha katiba ya klabu.
    8. Klabu hazijaambatanisha ripoti ya fedha ya mwaka.
    9. Klabu hazijajaza fomu ya kuthibitisha kushiriki mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom.
    Kwa taarifa hii kwa umma, Kamati ya Leseni ya Klabu inazitaka klabu kukamilisha vigezo hivyo kabla ya Septemba 22, mwaka huu. Vinginevyo, klabu  inaweza kuondolewa kwenye mashindano.
    Wakati huo huo: TFF imetoa maelekezo ya kufuatwa kwa utaratibu wa mawasiliano kwa mfumo wa halakia  yaani ngazi moja baada ya nyingine kwa ukubwa.
    Mawasiliano hayo yanalenga zaidi katika kualika viongozi wa kitaifa wa TFF katika programu au shughuli mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu hapa nchini.
    “TFF ingependa kuelekeza kuwa kama kuna suala la mwaliko au barua ya kwenda viongozi wa juu kuanzia kwa wadau, ngazi ya wilaya na mkoa kupita hatua moja baada ya nyingine kabla ya kufika katika ofisi ya Katibu Mkuu.
    Tungependa kwa pamoja tushirikiane kwa kuheshimu mamlaka za mpira wa miguu zilizoko kwenye maeneo husika badala ya kufanya mawasiliano ya moja kwa moja na viongozi juu,” imesema taarifa ya TFF.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMATI YABAINI MAPUNGUFU KIBAO LESENI ZA KLABU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top