• HABARI MPYA

    Friday, September 01, 2017

    ELLY SASII KUCHEZESHA MECHI YA STARS NA PUNDAMILIA KESHO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    REFA chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Elly Sasii ndiye atapuliza kipyenga katika mchezo wa kirafiki kati ya wenyeji, Taifa Stars na The Zebras wa Botswana kesho.
    Katika mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam waamuzi wasaidizi watakuwa Soud Lillah (Line 1) na Frank Komba (Line 2) wakati mwamuzi wa akiba (Forth Official) atakuwa Israel Nkongo.
    Mchezo huo utaanza saa 10.00 jioni unaochezwa chini utaratibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambako Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepanga Watazamaji waingie uwanjani kwa kiingilio cha Sh 10,000 kwa Jukwaa Kuu na Sh 5,000 kwa mzunguko.
    Elly Sasii akiwa kazini katika mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga
    Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga leo Ijumaa amezungumza na wanahabari kwenye Ukumbi wa Hosteli ya TFF, Karume jijini Dar es Salaam ambako amethibitisha kwamba kikosi chake kiko imara kwa mapambano.
    Kwa upande wa Kocha wa Botswana, David Bright amesema yeye ni kocha mpya na amejitahidi kuteua timu mpya yenye mchanganyiko wa vijana na wazoefu aliokuja nao kuwajaribu kwa nyota wa Kitanzania.
    Taifa Stars iko kambini na nyota wake akiwamo Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Elias Maguli (Dhofar FC/Oman), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya),Farid Mussa (CD Tenerif/Hispania) na Simon Msuva (Difaa El Jadidah ya Morocco).
    Wengine ambao wako kambini Hoteli ya Sea Scape iliyoko Kunduchi, Dar es Salaam ni makipa Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Young Africans).
    Pia wamo Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphas Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).
    Viungo ni Himid Mao - Nahodha Msaidizi (Azam FC), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Shiza Kichuya (Simba SC), wakati Washambuliaji ni Raphael Daud (Young Africans), Kelvin Sabato (Azam FC) na Emmanuel Martin (Young Africans).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ELLY SASII KUCHEZESHA MECHI YA STARS NA PUNDAMILIA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top