• HABARI MPYA

  Thursday, April 04, 2024

  YANGA KUENDELEA KUWAKOSA YAO, PACOME NA AUCHO KESHO DHIDI YA MAMELODI


  KOCHA wa Yanga, Muargentina Miguel Angel Gamondi amesema kwamba kesho anaweza kumpata mchezaji mmoja tu kati ya wanne aliowakosa kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
  Waliokosekana kwenye mchezo wa kwanza wa nyumbani ni mabeki Kibwana Shomari, Kouassi Attohoula Yao (Ivory Coast)na viungo Peadoh Pacome Zouazoua (Ivory Coast) na Khalid Aucho (Uganda.
  Yanga SC kesho watakuwa wageni wa Mamelodi Sundowns katika mchezo wa marudiano wa Robó Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Ijumaa kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Loftus Versfeld Jijini Pretoria.
  Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari leo Jijini Pretoria, Gamondi amesema anasubiri baada ya mazoezi ya mwisho leo Uwanja wa Loftus Versfeld kuona kama ataweza kumpata japo mchezaji mmoja wa kucheza kesho kati ya wale aliowakosa kwenye mechi ya kwanza Jumamosi iliyopita Dar es Salaam.
  "Ni kweli tunaiwaza nusu fainali ya CAF, lakini tunajali pia na usalama wa afya za wachezaji wetu pia. Young Africans haichezi mashindano haya peke yake," amesema Gamondi.
  Muargentina huyo ameongeza kwamba hawaandai wachezaji wake kwa ajili ya historia ya Mamelodi, bali anaandaa timu yake kutokana na dakika 90 na ana imani na kazi waliyoifanya kwenye Uwanja wa mazoezi.
  "Tuna Wachezaji wenye uzoefu wenye sifa ya kupambana, msimu uliopita kwenye Fainali ya Kombe la Shirikisho walipoteza nyumbani lakini wote mnajua kilichotokea walipokwenda ugenini, kesho ni mchezo tofauti lakini watapambana tena kwa ajili ya mashabiki wetu," amesema Gamondi.
  Ameongeza kwamba utakuwa mchezo mgumu, kwani kwa sasa kila timu ina nafasi ya kushinda, hivyo watahakikisha wanapambana kupata matokeo mazuri.
  "Mechi yangu ya mwisho hapa Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Loftus, nilikuwa Kocha wa Platinum Stars na tuliifunga Mamelodi magoli 2-1. Nina heshima kubwa na Nchi hii, nimeishi vizuri na watu wa hapa Lakini kwa sasa nimerudi na Young Africans SC na tunataka kuwafurahisha watu wa Watanzania," amesema Gamondi.
  Kwa upande wake, winga raia wa Afrika Kusini, Mahlatse 'Skudu' Manoka Makudubela aliyewawakilisha wachezaji wenzake wa Yanga amesema wamejiandaa vizuri na wako tayari kupambana kwa ajili ya timu. "Kila atakayepewa nafasi kwenye mechi ya kesho atajitoa kuhakikisha tunapata matokeo mazuri hapa," amesema Skudu.
  Yanga inahitaji ushindi au sare ya mabao ili kwenda Nusu Fainali kufuatia sare ya bila kufungana kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa jumla katí ya Esperance ya Tunisia na ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KUENDELEA KUWAKOSA YAO, PACOME NA AUCHO KESHO DHIDI YA MAMELODI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top