• HABARI MPYA

  Monday, May 09, 2022

  YANGA YATOA SARE TENA, 0-0 NA PRISONS, MAYELE...


  WENYEJI, Yanga SC wamelazimishwa sare ya bila kufungana na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Mshambuliaji Mkongo, Fiston Kalala Mayele atalala na mawazo leo baada ya kuikosesha nafasi mbili nzuri Yanga za kupata mabao kipindi cha kwanza.
  Kwanza alipewa pasi nzuri na kiungo Feisal Salum dakika ya 12, lakini akashindwa kufanya maamuzi ya haraka hadi beki wa Prisons akatokea na kuondosha kwenye hatari.
  Baadaye dakika ya 39 akaenda kupiga juu mkwaju wa penalti kufuatia Feisal kuangushwa kwenye boksi.

  Kwa sare hiyo ya tatu mfululizo, Yanga inafikisha pointi 57 katika mchezo wa 23 na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi 11 zaidi ya mabingwa watetezi, Simba ambao wenyewe wana mechi moja mkononi.
  Tanzania Prisons inafikisha pointi 23, mechi ya 23 nafasi ya 14 kwenye ligi ya timu 16, ambayo mwisho wa msimu mbili zitashuka na mbili zitakwenda kumenyana na timu za Championship kuwania kubaki Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YATOA SARE TENA, 0-0 NA PRISONS, MAYELE... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top