• HABARI MPYA

  Monday, May 23, 2022

  MAYELE AFUNGA LA 14, YANGA 1-1 BIASHARA KIRUMBA


  WENYEJI, Biashara United wamelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na vigogo, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
  Yanga walitangulia na bao la mshambuliaji wake Mkongo, Fiston Kalala Mayele dakika ya 75, kabla ya Collins Opare kuisawazishia Biashara United dakika ya 78.
  Mayele anafikisha mabao 14 na kumfikia mshambuliaji wa Geita Gold, George Mpole katika kinyang’anyiro cha ufungaji Bora.
  Yanga inafikisha pointi 64 katika mchezo wa 26 na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi 13 zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi.
  Biashara United wenyewe wanafikisha pointi 24 katika mchezo wa 25 na kupanda nafasi ya 14 kwenye ligi ya timu 16, wakiizidi wastani wa mabao tu Tanzania Prisons.
  Ikumbukwe timu mbili zitateremka moja kwa moja na mbili zitakwenda kumenyana na timu za Championship kuwania kubaki Ligi Kuu.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAYELE AFUNGA LA 14, YANGA 1-1 BIASHARA KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top