• HABARI MPYA

  Sunday, October 17, 2021

  RUVU SHOOTING YAICHAPA COASTAL UNION 1-0

  BAO pekee la Saadat Mohamed dakika ya 61 limeipa Ruvu Shooting ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Kwa ushindi huo, Ruvu Shooting inayofundishwa na kocha mzoefu, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ inafikisha pointi sita baada ya mechi tatu za mwanzo kufuatia kufungwa 1-0 na Dodoma Jiji FC Jijini Dodoma na kushinda 1-0 dhidi ya Biashara United mjini Musoma na leo ikicheza nyumbani kwa mara ya kwanza msimu huu inang’ara.
  Hali si nzuri kwa Wagosi wa Kaya ambao leo wamekamilisha mechi tatu bila ushindi kufuatia sare mbili za nyumbani 1-1 na Azam FC na 0-0 na KMC Uwanja wa Mkwakwani Jijiji Tanga.


  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Mbeya Kwanza imelazimishwa sare ya 0-0 na Dodoma Jiji Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
  Mbeya Kwanza inafikisha pointi tano baada ya mechi tatu, ikitoka kushinda 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini na sare nyingine ya 2-2 dhidi ya mahasimu wao wa Jiji, Mbeya City, wakati Dodoma Jiji baada ya kuichapa Ruvu 1-0 nayo ilichapwa 1-0 na Simba nyumbani, Uwanja wa Jamhuri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RUVU SHOOTING YAICHAPA COASTAL UNION 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top