• HABARI MPYA

    Friday, October 22, 2021

    BOCCO MCHEZAJI BORA LIGI KUU, FEISAL ASFC


    NAHODHA wa Simba SC, John Raphael Bocco ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita, wakati kiungo wa Yanga, Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Kombe la TFF, maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).
    Katika sherehe za utoaji tuzo hizo zilizofanyika ukumbi wa kituo cha Kimataifa cha mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, Bocco amewashinda aliyekuwa mchezaji mwenzake, kiungo Mzambia Clatous Chota Chama ambaye kwa sasa anachezea RS Berkane ya Morocco na kiungo wa Yanga, Mkongo Tonombe Mukoko.
    Kwa upande wake Mzanzibari, Feisal Salum  amewashinda Bocco na kiungo wa kimataifa wa Msumbiji, Luis Miquissone aliyekuwa Simba kabla ya kuhamia Al Ahly ya Misri.
    Aishi Manula wa Simba amebeba tuzo zote mbili za Kipa Bora wa Ligi Kuu na ASFC akiwashinda Jeremiah Kisubi aliyekuwa Tanzania Prisons kabla ya kuhamia Simba na Haroun Mandanda wa Mbeya City kwenye Ligi Kuu.
    Katika ASFC Aishi amewashinda 
    Mkenya Faroukh Shikhalo aliyekuwa Yanga kabla ya kuhamia KMC na Mganda Cleo James Ssetuba wa Biashara United.
    Mlinzi wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wa ameshinda Tuzo ya Beki Bora wa Ligi Kuu dhidi ya mchezaji mwenzake wa Simba, Shomary Kapombe na Dickson Job wa Yanga.
    Mshambuliaji Abdul Suleiman ‘Sopu’ wa Coastal Union ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi dhidi ya Dickson Job Yanga, Lusajo Mwaikenda wa KMC na Deogratius Mafie wa Biashara United).
    Kocha Bora wa Ligi Kuu ni Mfaransa, Didier Gomes wa Simba amewaangusha Mzambia George Lwandamina wa Azam FC na Mkenya Francis Baraza aliyekuwa Biashara United kabla ya kuhamia Kagera Sugar.
    Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Wanawake ni Amina Bilal aliyewashinda mchezaji mwenzake wa Yanga Princess, Aisha Masaka na Oppah Clement wa Simba Queens.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOCCO MCHEZAJI BORA LIGI KUU, FEISAL ASFC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top