• HABARI MPYA

  Monday, September 04, 2017

  TAMBWE, CHIRWA WAANZA MAZOEZI MEPESI YANGA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  WASHAMBULIAJI wa Yanga, Mrundi Amissi Tambwe na Mzambia, Obrey Chirwa wanaweza wakarudi kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Njombe Mji mwishoni mwa wiki.
  Hiyo inafuatia wawili hao kuanza mazoezi mepesi leo asubuhi chini ya uangalizi wa daktari katika kujaribu kuwafanya warejee mwishoni mwa wiki.
  Wakati Chirwa hajafanya mazoezi kabisa msimu huu kutokana na maumivu, Tambwe naye alitonesha goti katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Jamhuri wiki mbili zilizopita Uwanja wa Gombani, Pemba.
  Amissi Tambwe anaweza wakarudi kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Njombe Mji mwishoni mwa wiki

  Pamoja na hayo, kipa Benno Kakolanya na winga, Geoffrey Mwashiuya nao leo wameanza mazoezi mepesi baada ya kupona maumivu yaliyokuwa yakiwasumbua.
  Wawili wote wote wamekuwa nje ya Uwanja kwa maumivu tangu mwanzoni mwa msimu na sasa wanapambana kurejea uwanjani.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Dissmas Ten ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba wachezaji hao wataendelea na mazoezi mepesi kwa wiki moja zaidi kabla ya kujiunga na wenzao kwa programu kamili ya mazoezi.
  “Benno na Mwashiuya wameanza mazoezi mepesi na wataendelea hivi kwa wiki moja hadi hapo watakapojiunga na wenzao kwa programu kamili za mazoezi,”amesema Ten.
  Yanga SC imeendelea na mazoezi leo asubuhi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Njombe Mji Jumamosi Uwanja wa Saba Saba.
  Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina aliyekuwa kwao Zambia kwa ajili ya mazishi ya baba yake, amerejea jana na leo ameongoza mazoezi Uwanja wa Uhuru.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAMBWE, CHIRWA WAANZA MAZOEZI MEPESI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top