• HABARI MPYA

  Saturday, September 09, 2017

  NYONI, BOCCO WAAHIDI KUISAIDIA SIMBA KUSHINDA CHAMAZI

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  WACHEZAJI wapya wa Simba, beki Erasto Edward Nyoni na mshambuliaji John Raphael Bocco wamesema kwamba Uwanja wa Azam Complex, Chamazi ni sehemu amabyo wamecheza kwa muda mrefu na hawana shaka watafanya vizuri leo wakirejea kwa mara ya kwanza tangu wahame klabu yao ya zamani, Azam FC.
  Wakizungumza jana kuelekea mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, Bocco na Nyoni kwa pamoja wameahidi kuisaidia Simba kupata ushindi Azam Complex dhidi ya timu yao ya zamani.
  Bocco alienda mbali zaidi akasema anatamani kufunga bao leo kwenye Uwanja huo, ingawa akasema kuhusu kushangilia au kutoshangilia ataangalia hisia zitakavyomtuma baada ya kufunga.
  Erasto Nyoni ameahidi kuisaidia timu yake mpya, Simba kubeba pointi tatu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi 

  “Suala la kushangilia itategemea sasa, mtu pale pale unapofunga ndiyo unajua kama utashangilia au hushangilii,”alisema Bocco.
  Nyoni alisema anatarajia utakuwa mchezo mgumu, kwa sababu Azam FC nao wamejizatiti kwa kusajili wachezaji wengine wazuri, lakini akaseam anaipa nafasi kubwa timu yake mpya kuibuka na ushindi.
  “Sisi tutashinda kwa sababu kwanza tuna timu bora kuliko wao na pili hamasa ya mashabiki wetu, kutakuwa na watu wengi sana wanaotusapoti pale uwanjani siku hiyo,”alisema.    
  Ikumbukwe mchezo huo umerudishwa Saa 10:00 jioni kutoka Saa 1:00 usiku baada ya Jeshi la Polisi Tanzania kusema kwamba ni hatari mechi hiyo kuchezwa usiku.
  Refa Ludovick Charles wa Tabora ndiye atakayepuliza kipyenga katika mchezo huo, akisaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Abdallah Mkomwa wa Pwani na mezani atakuwepo Josephat Bulali na Kamisaa  atakuwa Ruvu Kiwanga, wote wa Dar es Salaam, wakati viingilio ni Sh. 10,000 kwa jukwaa la VIP na 7,000 kwa mzunguko.
  Timu zote zilishinda mechi zao za kwanza za Ligi Kuu, Azam FC wakiwachapa 1-0 wenyeji Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara na Simba wakivuna mabao 7-0 mbele ya Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NYONI, BOCCO WAAHIDI KUISAIDIA SIMBA KUSHINDA CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top