• HABARI MPYA

    Sunday, April 10, 2016

    SKENDO HII IMEINUKISHA TFF, TUIACHE TAKUKURU IFANYE KAZI YAKE

    MJADALA mkubwa katika vyombo vya habari wiki hii ni kashfa ya maofisa wa kuajiriwa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuomba rushwa ya Sh. Milioni 10 ili waisaidie timu ya Daraja la Kwanza.
    Kashfa hiyo imevuja kwenye mitandao ya kijamii kupitia sauti zilizorekodiwa wakati wa kikao cha pamoja cha maofisa hao wa TFF na viongozi wa klabu hiyo.
    Kwa mujibu wa sauti zile, Maofisa wa TFF walikuwa wanawaomba rushwa ya Sh. Milioni 10 klabu hiyo ili waisaidie mpango wa kumchongea mchezaji wa klabu nyingine, ambaye wanadai japokuwa mgeni, lakini anacheza kama mzawa.

    Sauti ya Ofisa wa TFF, inayofananishwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano, Martin Chacha inasikika ikiomba dau la Milioni 10 ili washinikize kikao cha kujadili uhalali wa mchezaji huyo.
    Na sauti hiyo inayodhaniwa kuwa ya Chacha inasikika ikiwapa matumaini viongozi wa klabu hiyo kwamba kuna mushkeli kweli kwenye vielelezo vya usajili wa mchezaji huyo.
    Sauti nyingine inayofananishwa na Juma Matandika, Msaidizi binafasi wa Rais wa TFF, Jamal Malinzi inasikika ikimtaja rais huyo.
    Sauti hiyo inayodhaniwa kuwa ya Matandika inasikika ikisema amekwenda kwenye kikao hicho baada ya kukataa wito wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi. Dioniz na Jamal ni mtu na kaka yake.
    Sauti inayofananishwa na Matandika inasikika ikisema amemdanganya Dioniz kwamba anakwenda kufanya kazi ya Rais (Jamal), ili kupata wasaa wa kuhudhuria kikao hicho.
    Ndani ya sauti hizo pia kuna sauti ya chini mno inayodhaniwa kuwa ya Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa. Kweli, kwa kawaida Mwesigwa huongea kwa sauti ya chini na kwa sababu katika rekodi hiyo sauti yake inasikika kwa mbali mno, imekuwa vigumu kwake kutajwa kwa uhakika kama wengine, yaani Chacha na Matandika. 
    Gazeti moja la kila siku lilipata ujasiri wa kipekee kwa kuthubutu kumtaja Mwesigwa naye alikuwepo kwenye kikao. Siku hiyo hiyo, Mwesigwa akawatishia kuwapeleka Mahakamani sambamba na kukana kuhusika.
    Chacha ameacha kazi siku moja baada ya kuvuja kwa sauti hiyo na Matandikwa amesimishwa kazi kupisha uchunguzi.
    Na sakata hili liliibuka siku chache baada ya Kamati ya Nidhamu ya TFF, chini ya Makamu wake Mwenyekiti, Wakili, Jerome Msemwa kutoa maamuzi ya shauri la upangaji wa matokeo yamechi za mwisho Kundi C kwa Ligi Daraja la Kwanza.
    Wakili Msemwa alisema Geita Gold yab Geita, JKT Oljoro ya Arusha na Polisi ya Tabora zimekutwa na hatia ya upangaji wa matokeo na kupewa adhabu ya kushushwa daraja mpaka ligi daraja la pili (SDL) msimu ujao.
    JKT Kanembwa FC ya mkoani Kigoma, imeshushwa daraja mpaka kwenye ngazi ya ligi ya mkoa (RCL), baada ya kushika nafasi ya mwisho katika msimamo wa kundi lake, Kundi C.
    Kamati pia ikawafungia maisha kutojihusisha na soka refa wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC v Geita Gold, Saleh Mang’ola na kamisaa wa mchezo huo Moshi Juma baada ya kukutwa na hatia ya upagaji matokeo.
    Aidha kamati pia imemkuta na hatia kocha msaidizi wa klabu ya Geita Gold, Choke Abeid na kumfungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu
    Makipa Mohamed Mohamed wa JKT Kanembwa na Dennis Richard wa Geita Gold wamefungiwa miaka 10 sambamba na kulipa faini ya Sh Milioni kumi (10,000,000) kila mmoja.
    Mwenyekiti wa Chama cha Soka Geita (GEREFA), Salum Kurunge, Mwenyekiti wa klabu ya Geita Gold, Cosntantine Moladi na Katibu wa klabu ya JKT Kanembwa Basil Matei wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu baada ya kutokutwa na hatia katika shauri hilo.
    Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tabora, Yusuph Kitumbo, Katibu wake, Fateh Remtullah, Mwenyekiti wa JKT Oljoro, Amos Mwita na kocha msaidizi wa Polisi Tabora, Bernad Fabian wamefungiwa maisha pia.
    Refa wa mchezo kati ya Polisi Tabora na JKT Oljoro, Masoud Mkelemi na refa wa akiba, Fedian Machunde wamefungiwa kwa miaka 10 na kutozwa faini ya Sh Milioni 10 kila mmoja.
    Katibu wa Polisi Tabora, Alex Kataya, Katibu wa JKT Oljoro, Hussein Nalinja, mtunza vifaa wa wa Polisi Tabora, Boniface Komba, na Meneja wa timu ya  Polisi Tabora, Mrisho Seleman, wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu ya baada ya kutokutwa na hatia.
    Kutokana na maamuzi hayo ya Kamati ya Nidhamu ya TFF, Kamati husika zitakaa kupitia Kanuni na kutangaza timu itakayopanda Ligi Kuu (VPL) msimu ujao na timu zitakazopanda Ligi Daraja la Kwanza (StarTimes) msimu ujao.
    Ikumbukwe Rais wa TFF, ndiye aliyetoa tamko la kusitisha matokeo ya kutisha mechi hizo za mwisho za Daraja la Kwanza Kundi C na kuamuru mamlaka zifanye uchunguzi.
    Baada ya masuala haya kufuatana, maamuzi ya kesi ya upangaji matokeo na kuvuja kwa rekodi za sauti zinazodaiwa kuwa za Maofisa wa TFF wakiomba rushwa ya Sh. Milioni 10, watu wamekasirika mno.
    Baadhi wanasema Malinzi ajiuzulu kwa kashfa hii wakitoa mifano ya sakata la FIFA hivi karibuni, lililosababisha kwa Rais wa muda mrefu, Sepp Blatter kubwaga manyanga.
    Ukweli ni kwamba kashfa hii ni mbaya kwa TFF, lakini ipo haja ya watu kutofautisha mambo badala ya kushauri kwa jazba.
    Blatter akiwa Rais wa FIFA, alikutwa na skendo ambazo zilikuwa maamuzi ya FIFA kama kuuza haki za matangazo ya Televisheni na kutoa uenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia 2010 Brazil baada ya kupokea rushwa.
    Kiungwana, baada ya kuvuja kwa mkanda mzima, Blatter na wenzake wote hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kujiuzulu. Yalikuwa makosa yao.
    Lakini katika kesi inayoendelea, wahusika ni waajiriwa wa TFF na hakuna sauti hata moja inayofananishwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji au kiongozi yeyote wa kuchaguliwa wa TFF kuhusika kwenye kikao hicho.
    Sauti inayofanana na Matandika kumtaja Malinzi! imemtaja kweli, lakini inavyoonekana bwana mkubwa huyo alitaka kutumia ukaribu wake na Rais wa TFF kufanikisha mpango wao wa kuomba rushwa ya Sh. Milioni 10. Kama kweli ilikuwa sauti yake.
    Nasema kama kweli ilikuwa sauti yake kwa sababu sitaki kuingilia uchunguzi ambao unafanywa hivi sasa na vyombo vya dola, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
    Ukweli ni kwamba kashfa hii ni mbaya na inaitia doa TFF, lakini pia ipo haja ya kuweka jazba kando na kuviachia vyombo vya dola vifanya kazi kwa sasa.
    Nina imani sana na TAKUKURU kwa maana zote, uwezo wa kufanyia kazi suala hili na uaminifu pia kwamba hawawezi kughilibiwa kwa namna yoyote wakathubutu kuwalinda watu ambao si waadilifu.
    Inawezekana kweli sauti inayofananishwa na Matandika ilimtaja Malinzi kwa sababu alikuwa anahusika kwenye mpango huo – lakini shaka juu ya hilo itaondolewa na TAKUKURU.
    Sioni sababu ya kuwafundisha kazi TAKUKURU ikiwa tumekwishathibitishiwa kwamba tayari wameanza kulifanyia kazi suala hilo.
    Tuweke jazba kando na tuwaache TAKUKURU wafanya kazi yao bila kubughudhiwa, ili mwisho wa siku waje na majibu ya kututoa shaka juu ya sakata hili.
    Watuhumiwa wanadai sauti zao zilitengenezwa kwa minajili ya kuwachafua, nao wana haki – lakini kwa kuwa suala lipo mezani kwa TAKUKURU utetezi wao utageuka kuwa uongozi, ama kusimama kama kweli baada ya uchunguzi wa chombo hicho cha dola. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SKENDO HII IMEINUKISHA TFF, TUIACHE TAKUKURU IFANYE KAZI YAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top