• HABARI MPYA

    Thursday, July 02, 2015

    YANGA SC KUFANYA ‘BONGE LA PATI’ JUMAMOSI JANGWANI, JAYDEE, MSONDO NA YAMOTO KUTUMBUIZA

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    YANGA SC Jumamosi wiki hii watafanya tafrija ya kuazimisha miaka yake 80 sambamba na kutwaa ubingwa wa 25 wa LIgi Kuu ya Vodaxom Tanzania Bara msimu uliopita.
    Katibu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba sherehe zitafanyika makao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam kuanzia Saa 4:00 asubuhi.
    Dk Tiboroha amesema siku hiyo kutakuwa na burudani mbalimbali ikiwemo muziki na michezo na kwamba wanasiasa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri wamealikwa.
    Amesema bendi za Yamoto, Msondo na wasanii kama Lady Jaydee, Msagasumu na wengine watatoa burudani siku hiyo.
    Amesema wachezaji wote wa Yanga SC ambao hawamo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichokwenda Uganda watakuwapo.
    “Tutajumuita na wapenzi, mashabiki na wanachama wetu kushereheka miaka 80 ya Yanga SC pamoja na ubingwa wa 25 wa Ligi Kuu, nawaomba wana Yanga wote tukutane Jangwani Jumamosi,”amesema Dk. Tiboroha. 
    Kocha wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm akiwapa maelekezo wachezaji mazoezini leo
    Mshambuliaji Malimi Busungu akimlamba chenga kipa Deo Munishi 'Dida'
    Wachezaji wa Yanga SC wakiwa mazoezini leo Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam 
    Mabeki Pato Ngonyani kushoto na Edward Charles kulia wakiwania mpira.

    HII NDIYO YANGA:
    INGAWA historia inasema Yanga ilizaliwa mwaka 1935 na Simba mwaka 1936, lakini ukizama ndani utagundua kwamba, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa utani na upinzani wa jadi, baina ya miamba hiyo ya soka nchini.
    Kulikuwa kuna timu inaitwa New Youngs, ambayo mwaka 1938 ilisambaratika na baadhi ya wachezaji wake wakaenda kuunda timu iliyokuwa ikiitwa Sunderland, ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba.
    Kabla ya kutokea vurugu zilizoisambaratisha New Youngs, vijana wa Dar es Salaam walikuwa wana desturi ya kukutana viwanja vya Jangwani kufanya mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao, waliyoipachika jina Jangwani.
    Ndani ya kipindi kifupi tu, timu hiyo iliteka hisia za wengi, waliojitokeza kujiandikisha uanachama wa klabu hiyo. Miongoni mwa waliovutika na uanachama wa klabu hiyo ni Tarbu Mangara (sasa marehemu) na ilipofika mwaka 1926, walifanya mkutano wa kwanza katika eneo ambalo hivi kuna shule ya sekondari ya Tambaza.
    Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha timu hiyo, ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa Bandarini na mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo wa bandarini.
    Baada ya mkutano huo, timu hiyo ilibadilishwa jina na kuwa Navigation, iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za Waafrika enzi hizo, kabla ya uhuru wa Tanganyika. Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na Mtendeni zilikuwa hazifui dafu kwa wana Jangwani hao.
    Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama wa timu hiyo walikuwa wakitembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani, kwamba wao ndiyo zaidi. Kwa sababu katika kipindi hicho, Italia ilikuwa inatamba kwenye ulimwengu wa soka, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu yao na kuiita Taliana.
    Taliana ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza ilipopanda hadi Ligi Daraja la Pili Kanda ya Dar es Salaam, mwanzoni mwa miaka ya 1930. jina la Taliana waliamua kuachana nalo mapema, kabla ya kuingia kwenye ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
    Lakini kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya vitu pia, kwani wakiwa na jina la New Youngs, waliweza kutwaa Kombe la Kassum, lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam. 
    Hatimaye ukawadia mwaka mbaya kwa New Youngs, 1938 wakati baadhi ya wachezaji walipojitoa na kwenda kuanzisha Sunderland. Kwa sababu hiyo, waliobaki wakaamua kubadili jina na kuwa Young Africans, jina ambalo mashabiki wake wengi walishindwa kulitamka vizuri hivyo kujikuta wakisema Yanga.   
    Miaka 80 baadaye, leo Yanga SC ni timu ya kihistoria Tanzania, ikiwa inaongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, mara 25.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC KUFANYA ‘BONGE LA PATI’ JUMAMOSI JANGWANI, JAYDEE, MSONDO NA YAMOTO KUTUMBUIZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top