• HABARI MPYA

    Monday, April 06, 2015

    UNA NYIMBO ZAIDI YA 50, WIMBO MMOJA DAKIKA 30 ZA NINI JUKWAANI?

    Katika mambo ambayo huwa yananikera sana kwenye maonyesho ya bendi zetu ni pale wimbo unaporefushwa hadi wewe shabiki unabaki kujiombea kimoyomoyo wimbo huo uishe.
    Unausikiliza mpaka masikio yanachoka kuusikiliza, unatazama kinachofanyika jukwaani hadi unachoka kutazama, waimbaji au madansa watamaliza staili zote za uchezaji kiasi kwamba inawabidi warudie tena na tena kile ambacho wameshakifanya hapo kabla kupitia wimbo huo huo.
    Ni katika hatua hii ndipo utangundua kuwa unachokisikiliza au kukishuhudia hapo jukwaani ni tofauti kabisa na wimbo halisi ulivyorekodiwa, vitaongezwa vitu vingi ambavyo ni vigeni kwako ili mradi tu wimbo uwe mrefu.

    Siku moja rafiki yangu mmoja aliniambia alitoka kwenye show moja ya bonanza la kila Jumapili maeneo ya kinondoni akaenda hadi Ubungo stand kuu ya mabasi kumpokea mgeni wake, akampeleka nyumbani kwake Mwananyamala na kurejea tena kwenye bonanza hilo la bendi fulani na kukuta kinachondelea jukwaani ni wimbo ule ule aliouacha. Unaweza kumuona  kama mzushi lakini hiyo ndiyo hali halisi ya bendi zetu nyingi zinazojiita za kisasa.
    Ukiwauliza wanamuziki wengi ‘wa kisasa’ juu ya kurefushwa kwa nyimbo hadi kupitiliza watakupa majibu mepesi sana: “Hiyi ndiyo live …live lazima iwe tofauti na ilivyorekodiwa, lazima iwe ndefu ili watu wacheze”. Hayo ndiyo majibu yao.
    Kwa bahati mbaya sana, hata wamiliki wa bendi wameingia kwenye mtego huo huo, nakumbuka siku moja tajiri mmoja wa bendi fulani alipa majibu hayo hayo. “Hiyo ndio live”, alinijibu kirahisi kabisa.
    Nilitegemea kuwa wimbo ambao orijino yake ni dakika labda 10 basi jukwaani utakwenda kwa dakika 15 au 16, lakini kurefushwa hadi dakika 2o, 25 au 30 inahitaji mshabiki mwenye masikio na macho ya kijeuri ili kukubaliana na hali hiyo.
    Huwa nakubali hali hiyo kwa shingo upande pale tu ninapokutana na bendi mpya ambayo haina zaidi ya nyimbo nne, lakini kwa bendi yenye hazina ya nyimbo 50 au 70 ni kituko kung’ang’ania wimbo mmoja kwa nusu saa, ni kero, ni kukimbiza wateja.
    Katika kipindi hiki ambacho bendi nyingi zimekuwa zikilia na vyombo vya habari, ni muhimu kwao kuwa na program zitakazowashawishi mashabiki wao kurejea ukumbini onyesho hadi onyesho na si kuwatia uvivu au kuwakimbiza kabisa.
    Hebu angalia mahesabu haya mepesi: bendi nyingi zinaanza rasmi maonyesho saa 4 usiku hadi 9 hizo ni sawa na dakika 300 ambapo kama utapiga kila wimbo kwa dakika 25 bila matangazo au porojo zozote zile jukwaani basi zitapigwa nyimbo 12 tu au pungufu ya hapo.
    Kama unadhani hilo ni tatizo pekee basi andika maumivu, lipo tatizo lingine kubwa zaidi ya hilo ambalo ni lile la nyimbo hizo hizo 12 kujirudia katika kila onyesho, kama kutakuwa na badiliko basi ni kwa nyimbo moja au mbili.
    Ukichanganya tatizo la kwanza la nyimbo kurefushwa na hili la nyimbo za aina fulani kujirudia kila onyesho huwa nabaki nikijiuliza ni uvivu wa mazoezi? Ni kukosa ari ya kazi? Ni kukosa viongozi wenye mawazo chanya au ni kitu gani?
    Kwanini bendi yenye nyimbo 50 au 70 iwe inarudia nyimbo 10 kila onyesho? Kwanini irefushe nyimbo bila sababu za msingi?
    Hivi unategemea nini kwa mteja ambaye kila anapokuja kwenye maonyesho yako anakutana na nyimbo zilezile tena kwa mpangilio ule ule? Mteja anapofikia hatua ya kukariri program yako ya show kutokana na namna usivyotaka kubadilika matokeo yake ni lazima akukimbie.
    Watu wanakimbilia kwenye muziki wa disco kutokana na utundu wa madj kubadilika kama kinyonga wakihakikasha kuwa jana na leo zinakuwa ni siku mbili tofauti ambazo hazifanani kwa namna yoyote ile …wanamuziki, viongozi na wamiliki wa bendi chukueni hatua sasa kabla jahazi halijazama.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UNA NYIMBO ZAIDI YA 50, WIMBO MMOJA DAKIKA 30 ZA NINI JUKWAANI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top