• HABARI MPYA

    Monday, August 05, 2013

    BUSARA ITUMIKE KUINUSURU BAZA KWA MANUFAA YA MPIRA WA KIKAPU

    IMEWEKWA AGOSTI 5, 2013 SAA 9:55 ALASIRI
    TANGU kumalizika kwa mashindano ya mpira wa kikapu maarufu kwa jina la ‘Thabit Kombo Cup’ yanayofanyika kisiwani Pemba kila mwaka, hali ya hewa ndani ya chama cha mchezo huo Zanzibar (BAZA) si shwari.
    Kuchafuka kwa hali hiyo kumetokana na upande mmoja kutangaza mgogoro dhidi ya uongozi wa BAZA Taifa.
    Uongozi wa BAZA Pemba, umesema wazi kuwa, hauko tayari kushiriki mashindano yoyote yatakayoandaliwa na BAZA Taifa na hata ligi kuu ya Zanzibar , hadi pale Mwenyekiti na Katibu wake ngazi ya taifa watakapoachia ngazi. 

    Sababu zilizotolewa na viongozi hao ni kukiukwa kwa katiba ya chama walikodai kunafanywa na wenzao wa Unguja, pamoja na ubadhirifu wa fedha za udhamini wa mashindano ya Kombe la Thabit Kombo mwaka huu.
    Aidha, wamedai kuwa viongozi wa kitaifa, yaani Mwenyekiti na Katibu wake, wamekuwa wakihodhi mamlaka ya kufanya maamuzi peke yao kwa utashi binafsi, na kwa kuwatenga wenzao sambamba na kamati tendaji.
    Katika kusisitiza msimamo wao huo, viongozi hao wameuandikia uongozi wa kitaifa barua tangu Julai 17, mwaka huu, kuwataka wajiondoe vyenginevyo wataomba kuitishwa mkutano mkuu wa dharura wa chama kushindikiza kuondoka kwa viongozi hao.
    Huku BAZA Pemba ikisubiri majibu ya barua yao kutoka kwa viongozi wao wa Unguja, kumekuwa na taarifa kwamba tayari Mwenyekiti wa chama hicho ameandika barua ya kuomba kujiuzulu.
    Hata hivyo, Mwenyekiti huyo amesema hatua yake ya kutaka kuachaia ngazi haina uhusiano wowote na mambo yanavyokwenda sasa ndani ya chama hicho, na kupelekea wao kutakiwa kujiuzulu.
    Mwenyekiti huyo amedai kuwa uamuzi wake umetokana na kukosa muda wa kutekeleza majukumu yake ya kifamilia kwa kuwa shughuli za BAZA ni nyingi na zinamnyima nafasi ya kufanya mambo mengine muhimu. 
    Lakini pia, BAZA Pemba wanadai kuwa taarifa za kujiuzulu kwa Mwenyekiti wanazisikia kwenye vyombo vya habari, na wanasema kama ni hivyo, basi aondoke na Katibu wake.
    Kama hilo halitoshi, wanadai kuwa wamesikia BAZA Unguja wamefanya kikao na kuamua kumzuia Mwenyekiti asijiuzulu, na kusema kuwa kama kikao hicho kimefanyika, basi kilikuwa batili kwa kuwa kimekiuka vifungu vya katiba ya chama, kwa kutokuwa na mjumbe hata mmoja kutoka Pemba aliyehudhuria.
    Nina hakika hakuna hata mdau mmoja wa michezo ambaye anashabikia mvutano huo kati ya viongozi wa BAZA, kwani si wa manufaa kwa yeyote na unaweza kurejesha nyuma jitihada za kuendeleza mchezo wa mpira wa kikapu nchini.
    Ni ukweli usiofichika kwamba, panapokuwa na kundi la watu wanaounganishwa na harakati mbalimbali za kijamii ikiwemo uongozi au ushiriki wa michezo, hawawezi kuwa na fikra sawa, na lazima kutatokea misuguano ya hapa na pale.
    Lakini viongozi au wanachama wanapohitilafiana, ni muhimu warudi kwenye katiba za vyama vyao ambamo ninaamini ndimo mnamoweza kupatikana suluhu na kuleta maelewano kati yao .
    Kwa hivyo, viongozi wa BAZA wanapaswa kutambua kwamba huu ni wakati muhimu kwao kuimarisha chama chao kwa kuangalia zaidi mambo yanayowaunganisha na kuyaweka pembeni yake yanayowagawa. 
    Malalamiko haya yanayotolewa na viongozi na wajumbe wa kamati tendaji Pemba, si ya kupuuzwa hata kidogo kwani kama yataachiwa huenda ukawa mwanzo wa kusambaratika kwa chama na hivyo kuvuruga kabisa ndoto za vijana wanaopenda kucheza mpira wa kikapu kwa malengo maalum.
    BAZA Taifa inapaswa kutumia busara na kuitisha mkutano mkuu wa dharura haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuwekana sawa.
    Mivutano na migogoro kama hii ndani ya vyama vya michezo, haiashirii mustakbali mzuri kwa mchezo husika na wanamichezo wenyewe, na pia inawavunja moyo wafadhili wanaojitokeza kuibeba michezo hiyo.
    Ni jambo la kushukuru kwamba amejitokeza mdhamini wa mashindano ya Kombe la Thabit Kombo Pemba , ambaye tangu alipoanza kuyafadhili, amekuwa akiendelea kila mwaka.
    Kama kuna madai dhidi ya viongozi wa BAZA taifa kwamba wanavunja katiba, iko haja basi kamati tendaji ya chama hicho iliangalie hilo kwa jicho la tatu ili kusafisha hali ya hewa iliyoanza kuchafuka.
    Aidha, kama walivyodai viongozi wenza wanaofanyia kazi ofisi ya BAZA kisiwani Pemba , kwamba hawaridhiki na wenzao wa Unguja kufanya kikao cha kujadili ombi la Mwenyekiti kutaka kujiuzulu kwa kuwa hawakushirikishwa nao, nalo ni jambo linalohitaji kutazamwa kwa uzito mkubwa.
    Hata kama viongozi na wajumbe wa Pemba wanataka Mwenyekiti na Katibu wajiuzulu, mkutano wa kuijadili barua aliyowasilisha Mwenyekiti ilipaswa kukaliwa kitako na wajumbe wote wa kamati tendaji, na huu ndio utaratibu wa vyama vyote.
    Utaratibu huu unahitaji kufuatwa ili mkutano huo usihodhiwe na wajumbe wasioafiki ombi la kiongozi anayetaka kuachia ngazi peke yao , ambao katika hili, wanadaiwa kwamba wanakusudia kumlazimisha abaki, bali na wale wanaoafiki kwamba aondoke wakae pamoja nao.
    Hata pale wajumbe wengine wanapokosekana, lakini lazima akidi ya wajumbe wa mkutano mkuu ifikie kiwango kinachokubalika na chama husika.
    Madai yaliyotolewa na wajumbe wa BAZA Pemba kwamba Mwenyekiti na Katibu wake wanatumia madaraka yao kwa maslahi binafsi badala ya kuendeleza mpira wa kikapu Zanzibar ni mazito.
    Kama chama chenyewe kinashidwa kuitisha mkutano ili kutafuta dawa ya kunusuru mpasuko, Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, litie mkono wake kupitia Mrajis wa vyama vya michezo, kwani ninaamini sote tunaangalia zaidi katika kujenga kuliko kubomoa.
    Patafutwe wapi penye kasoro ili zirekebishwe kwani tunachokitaka ni maendeleo ya michezo na sio migogoro ndani ya vyama vinavyopaswa kuisimamia
    Tel:0777 865050
    E-mail: salumss@yahoo.co.uk
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BUSARA ITUMIKE KUINUSURU BAZA KWA MANUFAA YA MPIRA WA KIKAPU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top