• HABARI MPYA

    Monday, March 06, 2017

    MUNISI BOSI MPYA WA SOKA PWANI

    Na Gustaphu Haule, PWANI
    CHAMA cha Soka wilaya ya Kibaha (KIBAFA) kimepata safu ya viongozi wapya kufuatia uchaguzi wake mkuu uliofanyika juzi katika viwanja vya Seven Seven vilivyopo Miembesaba huku Robert Munisi akiibuka kuwa Mwenyekiti.
    Aidha, uchaguzi huo haukuwa na upinzani mkali kwakuwa wagombea wote hawakuwa na wapinzani na hivyo wengi wao kujikuta wakipita bila kupingwa kwa kupata kura zote za wajumbe 57 walioshiriki katika uchaguzi huo.
    Matokeo ya uchaguzi huo yalitangazwa jana na  makamu Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi kutoka chama cha mpira wa Miguu Mkoani Pwani (COREFA) Stephen Mwakibolwa, ambapo alimtaja Robert Munisi kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho.
    Mwenyekiti wa KIBAFA, Robert Munisi akizungumza katika uchaguzi huo 
    Mwenyekiti wa Chama Soka Pwani (COREFA), Hassan Hassanoo (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wapya wa Chama cha Soka Kibaha (KIBAFA),wa kwanza kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa KIBAFA, Daudi Mhina, wa pili ni Mwenyekiti wa KIBAFA, Robert Munisi na wa kwanza kutoka kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa KIBAFA, Rajabu Shebuge. PICHA NA GUSTAPHU HAULE

    Mwakibolwa, alisema katika safu hiyo nafasi ya makamu mwenyekiti wa Kibafa imechukuliwa na Rajabu Shebuge,aliyepata kura 57 huku nafasi ya katibu mkuu ikishikiliwa na Daudi Mhina(Morinho) aliyepata kura zote.
    Alisema, nafasi ya katibu msaidizi imechukuliwa na Ivan Lawrence, aliyepata kura za ndio 56 huku kura moja ikimkataa na Mweka hazina akiwa ni Mohamed Ally aliyepata kura 55 na mbili za hapana.
    Hata hivyo, nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu wa Corefa imekwenda kwa David Mgogo(57) huku mwakilishi wa vilabu akiwa Japhet John (Mzee wa Mbata) aliyepata kura 57.
    Akizungumza mara baada ya uchaguzi huo mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu Mkoa wa Pwani Hassan Hassanoo, aliwataka viongozi waliochaguliwa wawe chachu ya kuendeleza soka Wilayani Kibaha.
    Hassanoo, alisema kuwa katika kipindi cha miaka nane iliyopita Kibaha mpira ulikufa kutokana na kukosa viongozi wa kikatiba hivyo kwasasa anaimani soka la kibaha litaendelea kufanyika kikamilifu kama Wilaya nyingine.
    Alisema,viongozi hao wasiwe chanzo cha kuvuruga mpira na badala yake wazidi kuimarisha ili wadau wa mpira wapate moyo wa kuchangia zaidi lengo likiwa ni kukuza vipaji .
    "Nataka kuona timu zinazofanya vizuri kama Kiluvya United mwakani zinapanda ligi kuu lakini kupanda huko kutatokana na ushirikiano wa huku Kibafa hivyo tushirikiane kukuza soka la Pwani,"alisema Hassanoo.
    Kwa upande wake mwenyekiti wa Kibafa Robert Munisi ,alisema kuwa wapo tayari kukabiliana na changamoto za kisoka zilizopo Wilayani Kibaha lakini kikubwa ni ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali .
    Munisi, alisema kuwa mpira ili huweze kuchezwa unahitaji viongozi wenye kujitoa,hivyo yupo tayari kufufua upya mpira wa miguu kibaha ikiwa ni kuanzisha timu za vijana chini ya umri wa miaka 18 na kuendelea.
    Alisema,anachotaka ni kuona Kibafa kinakuwa chama cha mfano katika kuendeleza soka ili Wilaya nyingine zipate kuiga kutoka kwao na kwamba ataongoza chama hicho kwa kufuata katiba na msingi iliyowekwa kwa ajili ya kuimarisha soka.
    Munisi,alikiomba chama cha soka Mkoani Pwani (COREFA), kuendelea kushirikiana kikamilifu ili kuweza kutatua changamoto za kisoka kwa pamoja na kwamba mategemeo yao makubwa ni kupata muongozo kutoka COREFA.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MUNISI BOSI MPYA WA SOKA PWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top