• HABARI MPYA

    Thursday, April 06, 2023

    SIMBA WASIJISHUSHE, YANGA WASIJIDANGANYE KWA RIVERS


    DROO ya mechi za Robo Fainali ya michuano ya klabu barani Afrika imepangwa jana makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Jijini Cairo nchini Misri – na Simba watamenyana na mabingwa watetezi, Wydad Casablanca ya Morocco katika Ligi ya Mabingwa, wakati Yanga watacheza na Rivers United ya Nigeria katika Kombe la Shirikisho.
    Simba inarejea Morocco ambako katika mechi za Kundi C ilifungwa nyumbani na ugenini na vigogo wengine wa nchi hiyo, Raja Casablanca, 3-0 Dar es Salaam na 3-1 Casablanca.
    Kwa Yanga nao, hayo ni marudio ya mechi ya hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, walipotolewa na Rivers United kwa jumla ya mabao 2-0 ikifungwa 1-0 nyumbani na ugenini.
    Robo Fainali nyingine za Ligi ya Mabingwa ni Al Ahly ya Misri dhidi ya Raja Casablanca, CR Belouizdad ya Algeria dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na JS Kabylie ya Algeria pia dhidi ya Espérance ya Tunisia.
    Mechi za kwanza za Ligi ya Mabingwa Afrika zitachezwa kati ya Aprili 21 na 22 na marudiano kati ya Aprili 28 na 29 na za Kombe la Kombe la Shirikisho zitafuatia Aprili 30.
    Mshindi kati ya Wydad Casablanca na Simba SC atakutana na mshindi wa mchezo kati ya CR Belouizdad ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, wakati Yanga ikivuka Robo itakutana na mshindi kati ya Pyramids na Marumo Gallants mwezi Mei.
    Ratiba hiyo ya klabu zetu imepokewa kwa mitazamo tofauti, kwa mashabiki wa Simba wanaona kabisa wana mtihani mgumu mbele ya Wydad, mabingwa wa Afrika mara matatu, 1992, 2017 na 2022, mabingwa wa Kombe la Washindi Afrika 2002 na washindi wa Super Cup ya CAF mwaka 2018.
    Kwa Yanga wamekuwa wakijipa moyo kwamba hawana shughuli pevu mbele ya Rivers United, ambao matokeo yao mazuri katika Ligi ya Mabingwa ni Hatua ya 32 Bora msimu uliopita na zaidi ya kuishia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2017 – hii ni mara ya kwanza wanafika Robo Fainali.
    Simba wanaweza kuona wana mtihani mkubwa – lakini na wao ni timu ya kuogopwa barani Afrika kutokana na rekodi zake, ikiwemo kuwatoa mabingwa wa Afrika wa mwaka 2003, Zamalek Jijini Cairo kwa penati baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
    Simba na Wydad zinakwenda kukutana kwa mara ya pili kihistoria baada ya mwaka 2011 walipokutana katika mechi ya mkondo mmoja Jijini Cairo, Misri na kufungwa 3-0.
    CAF iliagiza mechi hiyo ichezwe baada ya Simba kushinda rufaa waliyomkatia beki wa TP Mazembe, Janvier Besala Bokungu, aliyevunja mkataba kinyume cha taratibu na klabu ya Esperance ya Tunisia.
    Simba walikata rufaa baada ya kutolewa na Mazembe katika Hatua ya 32 Bora ya Ligi ya Mabingwa wakifungwa 3-1 Lubumbashi na 3-2 Dar es Salaam. Na Mazembe walikuwa wamekwishatinga Robo Fainali baada ya kuitoa Wydad kwa jumla ya mabao 2-1, wakifungwa 1-0 Casablanca na kushinda 2-0 Lubumbashi.
    Wydad AC walikwenda hadi Fainali na kufungwa 1-0 na Espérance kwenye mchezo wa marudiano Novemba 12, Uwanja wa Olimpiki mjini Rades, kufuatia sare ya Novemba 6, mwaka 2011 Uwanja wa Mfalme Mohammed V Jijini Casablanca.
    Simba wenyewe waliangukia kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako walitolewa na DC Motema Pembe ya DRC kwa mabao 2-1.
    Kwa Yanga, wakati wanaamini wana kazi nyepesi mbele ya Rivers United wakumbuke pia hawana upepo mzuri wanapokutana na timu za Nigeria kwenye michuano ya klabu ya Afrika – hivyo wanahitaji kuipa uzito mechi hiyo kwa maandalizi mazuri ili wakavunje mwiko.
    Yanga imekutana na wapinzani watatu jumla wa Nigeria kihistoria kwenye michuano ya Afrika – pamoja na Rivers United, wengine ni Enugu Rangers na Kwara United na wote waliitupa nje ya mashindano ‘Timu ya Wananachi’ yenye maskani yake Jangwani, Dar e Salaam.
    Mwaka 1975 katika Ligi ya Mabingwa Yanga ilitolewa na Enugu Rangers katika Hatua ya 32 Bora kwa mabao ya ugenini, baada ya sare ya 0-0 Nigeria na 1-1 Dar es Salaam.
    Mwaka 1999 Yanga SC ilitolewa na Kwara United kwa jumla ya mabao 4-0 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, kikosini wakiwa na Ally Mayayi Tembele – sasa Naibu Mkurugenzi wa Mchezo, walichapwa 1-0 Nigeria na 3-0 Dar es Salaam.
    Na mwaka jana hadi kizazi cha dijitali kinakumbuka vipigo vya nyumbani na ugenini, 1-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam na 1-0 Uwanja wa Adokiye Amiesimaka mjini Port Harcourt, Rivers State viliiondoa mapema Yanga kwenye michuano ya Afrika.
    Ukweli ni kwamba hakuna timu dhaifu inayoweza kufika hadi Hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Afrika – wote Simba na Yanga wana wapinzani wagumu na wanapaswa kuzingatia hilo na kufanya maandalizi mazuri.
    Simba hawapaswi kujishusha eti wana mpinzani mgumu hawawezi kuvuka, kwa sababu kufikiria hivyo watakuwa wanajikatisha tamaa wenyewe, ambayo itaewaelekeza mlango wa kutokea kwa urahisi.
    Simba SC imezoeleka kama ni timu ya kuustajabisha ulimwengu wa soka Afrika tangu miaka ya 1970 wakiwa wanajivunia wachezaji kama Athumani Mambosasa, Mohamed Kajole, Athumani Juma Kalomba, Omar Chogo, Adam Sabu, Abbas Dilunga (wote sasa marehemu), Hassan Baraza, Khalid Abeid, Haidari Abeid na Abdallah Kbadeni walipofika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974. 
    Na Yanga hawapaswi kujiamini mno kwamba wao ni zaidi ya Rivers United na wanakwenda kulipa kisasi kwa kuifunga nyumbani na ugenini na kuitoa mashindanoni, kwa sababu historia haiwabebi na pia kipimo cha ubora au udhaifu ni uwanjani.
    Hawajawahi kuifunga Rivers United wala timu yoyote ya Nigeria waliyokutana nayo tangu mwaka 1975 kikosini wana mchezaji anaitwa Sunday ‘Computer’ Manara – leo wanapata wapi kiburi cha kujiaminisha wanashinda kwa urahisi.
    Nguvu zielekezwe kwenye maandalizi mazuri ya kisayansi na mipango ya kimpira ya ndani na nje ya Uwanja kuhakikisha timu zetu zote zinakwenda Nusu Fainali. Kila la heri, Simba na Yanga michuano ya Afrika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WASIJISHUSHE, YANGA WASIJIDANGANYE KWA RIVERS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top