• HABARI MPYA

  Monday, December 19, 2022

  NI MESSI NA ARGENTINA BINGWA KOMBE LA DUNIA 2022


  HATIMAYE Lionel Messi amefanikiwa kutwaa Kombe la Dunia baada ya ushindi wa Argentina wa penalti 4-2 kufuatia sare ya kufungana mabao 3-3 ndani ya dakika 120 Uwanja wa Lusail Iconic mjini Lusail nchini Qatar.
  Hilo linakuwa taji la kwanza la Kombe la Dunia kwa Argentina tangu mwaka 1986, timu ilipoongozwa na gwiji wa enzi hizo, Diego Maradona, sasa marehemu.
  Ilikuwa mechi tamu ya funga nikufunge, Argentina ikitangulia kwa mabao ya Messi kwa penalti dakika ya 23 na Ángel Di María dakika ya 36, kabla ya Kylian Mbappe kuisawazishia Ufaransa mabao yote dakika ya 80 kwa penalti na 81.
  Katika dakika 30 za nyongeza, Messi akaifungia tena Argentina dakika ya 108, kabla ya Mbappe kuisawazishia Ufaransa dakika ya 108.
  Kwenye mikwaju ya penalti waliofunga za Argentina ni Messi, P. Dybala, L. Paredes na G. Montiel, wakati waliofunga za Ufaransa ni Mbappé na R. Kolo Muani pekee, huku za K. Coman na A. Tchouaméni zikiokolewa na kipa Emiliano Martinez.
  Na baada ya mechi, Messi alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano, Martinez kipa Bora huku Mbappe akichukua ya Ufungaji Bora.
  Mbappe amefunga mabao manane na kuwapiku Messi, Mfaransa mwenzake Olivier Giroud na Julian Alvarez.
  Ikumbukwe juzi Croatia ilifanikiwa kumaliza nafasi ya tatu baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Morocco.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI MESSI NA ARGENTINA BINGWA KOMBE LA DUNIA 2022 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top