• HABARI MPYA

    Friday, September 06, 2019

    VITA YA SAMATTA NA BERAHINO KUENDELEA JUMAPILI TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NYASI za Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Jumapili wiki hii zitahimili vishindo vya mchezo mkali baina ya wenyeji, Tanzania na Burundi kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 Qatar.
    Baada ya sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Intwari mjini Bujumbura Jumatano, Taifa Stars na Int’hamba Murugamba zitakutana tena Jumapili na mshindi wa jumla ataingia kwenye moja ya makundi 10 kuwania kwenda hatua ya mwisho ya mchujo wa mbio za Qatar 2022.
    Timu 10 zitakazoongoza makundi hayo zitamenyana baina yao na washindi watano ndio watakaoiwakilisha Afrika kwenye Kombe la Dunia lijalo, Qatar. 

    Mbwana Samatta (wa pili kulia) na Saido Berahino (wa pili kushoto) kabla ya mechi ya Jumatano Bujumbura

    Jumapili ni siku ambayo, Manahodha Mbwana Ally Samatta wa Tanzania na Saido Berahino wa Burundi watakuwa na wajibu mwingine wa kuzipigania nchi zao katika medani ya soka.
    Washambuliaji hao ambao wote wanacheza Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji, Jumapili walikutana Uwanja wa Intwari lakini wote wawili hawakufunga.  
    Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Taifa Stars inayofundishwa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragijje ikitawala vizuri mchezo kabla ya wenyeji kufunguka mwishoni mwa kipindi hicho, mambo yalibadilika kipindi cha pili.
    Mshambuliaji wa Al Taawon ya Saudi Arabia, Cedric Amissi aliwatanguliza wenyeji kwa bao zuri dakika ya 78, akimalizia pasi ya wa jina lake, Amissi Mohammed wa NAC Breda ya Uholanzi kutoka upande wa kushoto, ambaye alifanikiwa kuwatoka kiungo wa ENNPI ya Ethioppia, Himid Mao na beki wa Simba SC ya nyumbani, Ramadhani Haruna Shamte.
    Kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Happugod Msuva akaisawazisjhia Tanzania dakika ya 84 akimalizia mpira uliorudi baada ya kumgonga beki wa Burundi, Frederic Nsabiyumva kufuatia pigo la Mao. 
    Samatta anayechezea klabu ya KRC Genk na Berahino wa Zulte-Waregem, zote za Ubelgiji kila mmoja anajua anatakiwa kufanya kitu Jumapili, na si kingine zaidi ya kuisaidia nchi yake isonge mbele katika mbio za Qatar.
    Tayari katika ligi ya Ubelgiji wamekwishakutana mara moja Jumamosi ya Agosti 10/ mwaka huu na Berahino akamtambia Samatta baada ya kuisaidia Zulte-Waregem kupata ushindi wa 2-0 ugenini Uwanja wa Luminus  Arena mjini Genk.
    Tena siku hiyo, Berahino naye yeye mwenyewe aliifungia bao la pili Zulte-Waregem dakika ya 78, baada ya mshambuliaji mwenzake, Mnorway Henrik Rorvik Bjordal kufunga la kwanza dakika ya sita.
    Samatta ana deni kwa Berahino, nalo ni kulipa kisasa cha kwenye Ligi ya Ubelgiji kwa kuisaidia Taifa Stars kuifunga Burundi Jumapili. Hiyo ni burudani nje ya burudani yenyewe ya mchezo wenye ushindani mkali.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VITA YA SAMATTA NA BERAHINO KUENDELEA JUMAPILI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top